Mtoto wa Lowassa achukua fomu kuwani ubunge Monduli

Muktasari:

Wengine waliochukua fomu ni Yona Laizer, Lobulu Kivuyo na Eric Ngwijo.


Arusha. Mtoto wa Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa Fred Lowassa ni miongoni mwa wanachama watano wa Chadema waliochukua fomu za kugombea ubunge jimbo la Monduli.

Aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Julius Kalanga alijiuzulu na kujivua uanachama wa Chadema na kuhamia CCM.

Katibu wa Chedema Kanda ya Kaskazini, Aman Golugwa akizungumza na Mwananchi leo Agosti 9  alisema Fred amechukua fomu na kurejesha.

Golugwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Arusha, aliwataja wagombea wengine ni Cecilia Ndosi ambaye ni Mwenyekiti Baraza la Wanawake wa Chadema mkoa Arusha na Diwani viti maalum.

Amesema wengine ni Yona Laizer, Lobulu Kivuyo na Eric Ngwijo.

Amesema wagombea hao watapigiwa kura za maoni katika kikao kitakachofanyika Jumamosi kata ya Migungani wilaya ya Monduli.

“Kikao hicho  kitaratibiwa na ofisi ya Kanda ya kanda ya kaskazini na baadaye majina kupelekwa kamati kuu,” amesema.

Golugwa amesema katika jimbo la Korogwe vijijini mgombea mmoja amejitokeza  ambaye ni Amina Saguti.

Wengine waliochukua fomu  kwa upande wa  Korogwe Vijijini lakini hawakurejesha  hadi ulipofika mwisho wa kurudisha fomu ni Aroan Mashuve na Dafi Dafi.

Golugwa amesema kikao cha kumjadili mgombea huyo kitafanyika Jumapili Korogwe.