Mtulia akabidhiwa kadi ya CCM

Muktasari:

  • Mtulia amesema anaamini hatajutia uamuzi wake wa kuondoka CUF.

Maulid Mtulia aliyejivua uanachama wa CUF na kupoteza ubunge wa Kinondoni, amekabidhiwa kadi ya CCM.

Mtulia amekabidhiwa kadi leo Jumatatu Desemba 4,2017 na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni, Aroun Maluma.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa kadi, Mtulia aliyejiondoa CUF Desemba 2,2017 amesema ataweza kuwatumikia wananchi zaidi kuliko alikokuwa.

Amesema Rais John Magufuli alipozindua ujenzi wa nyumba Magomeni Kota jijini Dar es Salaam alizungumza naye kuhusu maendeleo ya Kinondoni, jambo  lililoonekana ni kinyume kwa upinzani.

“Hili lilileta shida na kuonekana sikufanya sawa, nimeona nije huku kabisa kwa sababu ilikuwa ngumu kwangu kuwatumikia wananchi. CUF ina migogoro isiyokwisha, hujui ukae upande upi, inakuwa ngumu kuwatumikia waliokuchagua katika utendaji wa namna hii, nimeamua kuhama,” amesema Mtulia.

Amesema akiwa mbunge wa CUF alishindwa kufanya mambo mengi, tofauti na angekuwa CCM.

“Msaada wangu kwa wananchi katika utekelezaji wa majukumu yangu kwao nikiwa CUF ulikuwa mdogo, ninachowashauri uchaguzi ujao wasifanye makosa tena, wamchague wa CCM ili aweze kutatua kero zao,” amesema Mtulia.

Amesema anaamini hatajutia uamuzi wake na hajahamia CCM kufuata vyeo, hivyo hata akiambiwa awe msaidizi wa mjumbe wa nyumba 10 yupo tayari.

“Kama nafasi hiyo pia itakuwa imejaa sina shida nitarudi Rufiji kwenye asili yangu nikavue samaki,” amesema.

Mwenyekiti wa CCM Maluma amesema wanaotaka kuhamia chama hicho wanakaribishwa lakini wafuate utaratibu.

Mwenyekiti wa CCM Kata ya Tandale, Tamim Omary amesema kwa Mtulia kujiunga na chama hicho anaamini wengine wengi watahamia.

“Mtulia ninamfahamu ni kijana mtulivu na mwenye nidhamu, naamini wana CCM wenzangu mtafaidika na nidhamu yake,” amesema Omary.