Muhimbili kuwapandikiza figo wagonjwa watano mwezi huu

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk, Faustine Ndugulile (wa pili kushoto) akiongoza maandamano wakati wa madhimisho  ya siku ya Figo Duniani yaliofanyika jijini Dar es Salaam jana.Picha na Said Khamis

Muktasari:

  • Novemba 21 mwaka jana, MNH ilifanya upandikizaji wa kwanza kwa Prisca Mwingira (30) ambaye alichangiwa figo na mdogo wake, Batholomeo Mwingira (27) na kuahidi kuwafanyia upandikizaji wa kiungo hicho wagonjwa wengine wanne ifikapo Januari.

 Wizara ya Afya imetoa ufafanuzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kutoendelea na upandikizaji wa figo Januari, ikisema itafanya tiba hiyo kwa wagonjwa watano mwezi huu na wengine saba ifikapo Aprili.

Novemba 21 mwaka jana, MNH ilifanya upandikizaji wa kwanza kwa Prisca Mwingira (30) ambaye alichangiwa figo na mdogo wake, Batholomeo Mwingira (27) na kuahidi kuwafanyia upandikizaji wa kiungo hicho wagonjwa wengine wanne ifikapo Januari.

Jana, mara baada ya matembezi ya hisani ya kilomita tano kuadhimisha Siku ya Figo Duniani, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile alimwambia mwandishi wetu kuwa kusitishwa kwa upandikizaji huo kulitokana na changamoto zilizojitokeza awali.

Alisema upandikizaji huo ulisimamishwa ili kuhakiki mifumo yake licha ya kwamba upasuaji wa awali ulifanyika kwa mafanikio.

“Tulihitaji muda zaidi wa uangalizi na kurekebisha baadhi ya vitu kwani baada ya upasuaji ilionekana kuna maeneo ambayo tulihitaji tuyaboreshe zaidi. Naamini wataalamu wetu wameshakamilisha na tunajipanga sasa kuendelea na upandikizaji,” alisema Dk Ndugulile na kuongeza:

“Lakini sambamba na hilo, Hospitali ya Benjamin Mkapa pia tunataka ianze kufanya upandikizaji wa figo na kwa bahati nzuri tuna madaktari wazuri wenye uwezo mkubwa wa kupandikiza.”

Rais wa Chama cha Madaktari wa Figo Tanzania ambaye pia ni daktari bingwa wa figo MNH, Onesmo Kisanga kuhusu hilo alisisitiza, “Kwa kuongezea tu mwezi huu tutawafanyia upandikizaji wagonjwa watano na mwezi ujao tutawapandikiza saba kwa kushirikiana na wenzetu, lakini kila mwezi tumepanga kumfanyia upandikizaji mgonjwa mmoja.”

Madaktari 100 kusomeshwa

Ili kukabiliana na tatizo la uchache wa wataalamu hao, Dk Ndugulile alisema Serikali imejipanga kusomesha madaktari bingwa wa figo 100 kila mwaka.

Alisema kuwa Serikali imeongeza wigo wa kutoa huduma za matibabu ya ugonjwa wa figo nchini kwa kuongeza vituo vya usafishaji damu hadi kufikia zaidi ya 17 na kuendesha mafunzo kwa madaktari bingwa ili kuwaongezea nguvu madaktari bingwa 13 waliopo.

“Wataalamu tunao 13 kwa upande wa madaktari, tumeiona hiyo changamoto kama Serikali, tumeongeza wigo wa kufanya mafunzo kwa madaktari bingwa na hivi karibuni tutatangaza ufadhili kupitia Serikali. Vilevile, tumetenga fedha kwa ajili ya kuwafundisha madaktari ili kutoa matibabu ya figo.

“Tumeongeza wigo wa usafishaji damu. Hadi tunavyoongea, tuna vituo zaidi ya 17 ambavyo vinatoa huduma ya kusafisha damu katika hospitali binafsi pamoja na hospitali zetu za Serikali, Muhimbili kuna vitanda 42, Mloganzila kuna vitanda 12, Bugando vitanda sita, KCMC vitanda sita, Mbeya vitanda sita, bila kusahau Regency, TMJ, Agakhan, Hindumandal na tunaendelea kuimarisha huduma.”

Alisema huduma za usafishaji wa damu kwa wagonjwa wa figo kwa sasa zinapatikana katika hospitali hizo za kanda, lakini kutokana na wagonjwa kuwa katika sehemu mbalimbali nchini, wataalamu hao wanahitajika kuwapo kwenye hospitali za rufaa za mikoa.

“Tukiwa na madaktari wawili kila mkoa tunakuwa tumepiga hatua kubwa,” alisema.

Dk Kisanga alisema mbali ya kutoa matibabu, lengo kubwa la madaktari wa figo ni kuhakikisha wanaielimisha jamii ili kupunguza wagonjwa wanaofika katika hatua za mwisho na hivyo matibabu yake kuwa ya gharama kubwa.

Alitoa wito kwa Watanzania kuwa makini jinsi ya kuandaa vyakula majumbani, kwa kupunguza kiasi cha chumvi kwenye chakula na mafuta akisema hayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza magonjwa ya shinikizo la damu (hypertension), kisukari na unene wa kupindukia.

Sambamba na ushauri huo aliwahamasisha wananchi kujenga tabia ya kufanya mazoezi mara kwa mara kama mojawapo ya njia za kujikinga.

“Watanzania hatujui kula, tunakula bora chakula kuliko chakula bora, matumizi ya vyakula vya mafuta, matumizi ya chumvi nyingi, matumizi ya vilevi, matumizi ya sigara kama hayana ulazima, basi tupunguze, tutumie vyakula vilivyochemshwa na vilivyochomwa, bila kusahau kujenga utaratibu wa kufanya mazoezi angalau mara tatu kwa wiki kwa saa moja inatosha,” alisema.