Muhimbili yataja kinachowatesa wanaume wengi, Makonda aja na kampeni ya tezi dume

Muktasari:

Wanaume hao hufika kitengo cha wagonjwa wa nje (OPD) kwa ajili ya kusaka tiba ya matatizo hayo.

Wakati mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akiandaa mkakati wa kuwapima wanaume wanaoishi jijini hapa saratani ya tezi dume nyumba kwa nyumba, imefahamika kuwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) hupokea wanaume wengi wenye matatizo ya mfumo wa uzazi.

Wanaume hao hufika kitengo cha wagonjwa wa nje (OPD) kwa ajili ya kusaka tiba ya matatizo hayo.

Mkuu wa Mawasiliano kwa Umma na Huduma kwa Wateja wa MNH, Aminiel Aligaesha alisema jana kuwa, “kwenye kliniki yetu ya OPD kati ya idara inayoongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi ni ile ya wanaume wanaofika kutibiwa magonjwa ya mfumo wa mkojo (urology).”

Tezi dume ikoje?

Saratani hiyo huathiri tezi iliyo katika mfumo wa uzazi wa mwanaume ambayo ipo chini ya kibofu cha mkojo na kuzunguka sehemu ya juu ya mirija inayosafirisha mkojo kwenda kwenye kibofu.

Tezi hiyo ndiyo huzalisha majimaji yanayorutubisha na kusafirisha mbegu za kiume.

Mkakati wa Makonda

Makonda alisema jana kwamba atatumia wataalamu wa afya kufanya upimaji huo ili kukabiliana na tatizo hilo katika mkoa wake.

Pia, aliwatoa hofu wanaume kuwa hawatapimwa kwa kutumia vidole, bali kwa kuchukuliwa sampuli ya damu.

Akizungumza wakati akifungua warsha ya chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi (HPV) kwa wasichana wa miaka 14 iliyovishirikisha vyombo vya habari, wataalamu wa afya na viongozi mbalimbali wa dini na siasa, Makonda alisema watu wengi hugundulika wakiwa na ugonjwa huo katika hatua za mwisho ambazo husababisha kifo.

“Unakwenda kuaga, baada ya muda unapata taarifa kuwa mhusika alikuwa na tezi dume sasa unashangaa kumbe hili ni tatizo kubwa,” alisema.

Alifafanua kuwa hilo ndilo limemsukuma kuja na mpango huo alioutaja kuwa mkakati maalumu.

“Mungu akituwezesha katika mkoa wetu tupite kila nyumba kupima tezi dume na tutapata wataalamu wa kutosha. Nina uhakika na kampeni hii tukishamaliza hii ya kuchanja watoto wa miaka 14, tutahakikisha tunapita kila nyumba.

“Walio wengi walikuwa na imani potofu ya aina ya kipimo chenyewe lakini watalaamu wameshabadilisha, utakuwa ni upimaji mzuri usio na bugudha na utapata majibu yako vizuri, tuondoe hili tatizo la saratani hapa nchini,” alisema.

Chanjo ya HPV

Akizungumzia chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi (HPV), meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita alitoa wito kwa viongozi wa dini na wanasiasa kuunga mkono jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuhakikisha wanatoa elimu na kuwahamasisha wananchi kuwapeleka mabinti zao kupata chanjo hiyo.

Mratibu wa Chanjo ya Mama na Mtoto Mkoa wa Dar es Salaam, Ziada Sera alisema kuna vituo 270 vilivyotengwa kwa ajili ya kutoa chanjo hiyo katika wilaya tano.

Alisema chanjo hiyo itatolewa kwa wasichana 24,097 wenye miaka 14 katika Mkoa wa Dar es Salaam na inatarajiwa kuanza kesho katika vituo hivyo.

Ziada alisema wasichana hao wamepatikana baada ya kupitisha dodoso katika shule za msingi na sekondari mkoani hapa.

Alisema waliwapatikana katika maeneo tofauti ikiwemo kwenye makazi ya watu na watoto wa mitaani. “Tumeshapitisha dodoso mashuleni na majumbani tayari Wilaya ya Ilala tuna vituo 71, Ubungo 48, Kinondoni 65, Kigamboni 19 na Temeke tunavyo 48. Hivi vyote vitatoa huduma kwa nyakati zote za chanjo hii,” alisema Ziada.