Muhongo awapa Sh4.5 milioni waathirika wa upepo

Muktasari:

Msaada huo umetolewa na Waziri wa Nishati na Madini ambaye ni Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo baada ya kupokea orodha ya waathirika.

Musoma. Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Kihemba, Kata ya Ifurifu wilayani hapa Mkoa wa Mara, waliokumbwa na maafa ya kubomoka nyumba na kuezuliwa kwa upepo ulioambatana na mvua, wamepata msaada wa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya zaidi ya Sh4.5 milioni.

 

Msaada huo umetolewa na Waziri wa Nishati na Madini ambaye ni Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo baada ya kupokea orodha ya waathirika.

 

Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Fred Yona amesema maafa hayo yalitokea Oktoba 9 saa 3:00 usiku, nyumba 44 ziliezuliwa na upepo na nyingine zilibomoka.

 

Yona amesema katika maafa hayo hakuna mtu aliyepoteza maisha lakini baadhi walijeruhiwa na kwamba kati ya nyumba hizo, nne zinahitaji kujengwa upya kutokana na wamiliki kutokuwa na uwezo.

 

“Walioathirika zaidi na ambao wamepata msaada ni Nyakaita Magati, Nyabweke Mabere (80) na Tatu Richard ambaye ni mjane,” amesema Yona.

 

Profesa Muhongo amesema suala la maafa ni gumu kwa sababu linatokea ghafla hivyo mtu hawezi kujiandaa kwa ajili hiyo, kinachotakiwa ni kusaidiwa kwa waathirika ili kurejea maisha yao ya kawaida.

 

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Musoma, Yohana Mirumbe amewataka ndugu na jamaa wa waathirika hao kuhakikisha wanawasaidia kukarabati haraka nyumba hizo ili shida wanayoipata.

 

Katibu wa CCM Wilaya, Mercy Mollel licha ya kumshukuru mbunge huyo kwa msaada huo, amemtaka aendelee kuwa na moyo huo wa kuisaidia jamii inayomzunguka.