Mvietnam wa kucha za Simba atozwa Sh10 mil

Muktasari:

Adhabu hiyo ilitolewa jana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Aishiel Sumari mbele ya Wakili wa Serikali, Ignas Mwinuka na Wakili wa mshtakiwa, Gwakisa Sambo.

Moshi. Raia wa Vietnam, Hoang Trung (50) aliyepatikana na hatia ya kusafirisha meno 60 na kucha 261 za simba zenye thamani ya Sh300 milioni kwenda nchini Qatar wiki iliyopita, amehukumiwa kulipa faini ya Sh10 milioni.

Adhabu hiyo ilitolewa jana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Aishiel Sumari mbele ya Wakili wa Serikali, Ignas Mwinuka na Wakili wa mshtakiwa, Gwakisa Sambo.

Jaji Sumari alisema iwapo mshtakiwa atashindwa kulipa faini hiyo, atalazimika kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela.

Hata hivyo, ndugu zake wanaofanya kazi kampuni moja ya simu za mkononi nchini, walifanikiwa kulipa faini hiyo.

Raia huyo wa kigeni alipatikana na hatia ya kosa hilo Agosti 16, baada ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa Kilimanjaro, Joachim Tiganga kumtia hatiani kwa makosa manne yaliyoangukia katika makosa ya uhujumu uchumi.