Mvua kubwa kunyesha Oktoba

Muktasari:

TMA imetoa tahadhari kwa maeneno ambayo yanatarajiwa kunyesha mvua hizo, wananchi na kamati za maafa zichukue tahadhari ya kuboresha miundominu ya mifereji ya maji


Dar es salaam. Mamlaka ya Hali ya  Hewa Tanzania (TMA) imesema mvua kubwa zinatarajiwa kunyesha katika kipindi cha Oktoba hadi Novemba, 2018 katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Kaskazini mwa Morogoro na visiwa vya Unguja na Pemba, Zanzibar.

Wakati huo huo, mikoa ya Kagera, Geita na wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma inatarajia kupata mvua wastani na chini ya wastani.

Hayo yamesema leo Septemba 6, 2018 na Mkuregenzi Mkuu wa TMA, Dk Agness Kijazi alipokuwa akitoa utabiri wa msimu wa mvua za vuli zinazotarajiwa kuanza Oktoba hadi Desemba,2018 hasa kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.

Dk Kijazi amesema mvua zinatarajiwa kuanza mapema wiki ya nne ya Septemba,2018 zitakazonyesha juu ya wastani hadi wastani huku vipindi vya mvua vikitarajiwa kuongezeko Oktoba na Novemba, 2018 katika mikoa hiyo.

Amesema katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara zinatarajiwa mvua kunyesha wastani hadi juu ya wastani kuanzia wiki ya pili ya Oktoba na zinatarajiwa kuisha wiki ya pili ya Desemba,2018.

Mikoa ya Mara, Mwanza, Mara, Simiyu na Shinyanga zinatarajiwa kunyesha mvua wastani hadi juu ya wastani huku mikoa ya Kagera, Geita na wilaya ya Kibondo zinatarajiwa kunyesha mvua za wastani na  chini ya wastani.

Dk Kijazi amesema kipindi cha msimu wa mvua hizo hali ya unyevunyevu wa udongo na upatikanaji wa chakula vinatarajiwa kuimarika huku mazao yasiyohitaji maji mengi yanaweza kuathiriwa na hali ya unyevunyevu wa kupitiliza na kusababisha maji kutuama.

Amesema upungufu wa unyevunyevu unaweza kujitokeza katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani hivyo wakulima wanashauriwa kupanda mazao yanayotumia muda mfupi kukomaa na yanayostahimili ukame.

Wachimbaji wa madini katika migodi midogomidogo wameshauriwa kuwa makini kwani ongezeko la maji katika udongo linaweza kusababisha mmomonyoko wa ardhi.

Pia, mamlaka za miji pamoja na wananchi wanashauriwa kuchukua tahadhari kuhakikisha mifumo na njia za kupitisha maji zinafanya kazi ili kuepusha mafuriko kutokea na uharibifu wa miundombinu.

Menejimenti ya maafa imeshauriwa kuandaa mbinu za kukabiliana na mafuriko na majanga yatokanayo na mafuriko kama vile kuimarisha na kuweka rasilimali kwa ajili ya kukabiliana na maafa, kuandaa vikosi kazi na kamati za maafa na kuandaa maeneo kuhudumia waathirika.