Mvua za masika kuanza mwezi Machi

TMA YATAHADHARISHA UWEZEKANO WA MAFURIKO MVUA ZA MWEZI MACHI HADI MEI

Muktasari:

TMA yasema maeneo mengi yatanufaika na mvua hizo kutokana na hali ilivyothibitika katika maeneo hayo

 


Dar es Salaam. Mvua za wastani mpaka juu ya wastani zinatarajiwa kuanza kunyesha katika kipindi cha wiki ya kwanza ya mwezi Machi hadi Mei mwaka huu katika maeneo mengi hapa nchini.

Hayo yameelezwa leo Februari 15, 2018 na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Agnes Kijazi alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari kuhusu mwelekeo wa mvua katika kipindi cha msimu wa masika.

Amesema zinatarajia kuleta athari katika sekta mbalimbali kutokana na vipindi vifupi vya mvua kubwa vinavyoweza kusababisha mafuriko

Dk Kijazi ametoa ushauri kwa sekta mbalimbali kuchukua tahadhari na kujiandaa ili kutumia vyema utabiri huo hasa menejimenti za maafa.

Amesema ukanda wa Pwani ya Kaskazini ikiwemo mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza ya Machi.

“Mvua hizi zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo hayo na Kusini mwa Mkoa wa Tanga, maeneo yaliyosalia yaliyo Kaskazini mwa Mkoa wa Tanzania yanatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani,” amesema Dk Kijazi.

Aidha, Dk Kijazi ameshauri wananchi kutumia kipindi hiki kuhakikisha wanafanya kilimo na usalama wa chakula, mifugo na wanayamapori.