Mwanri, Kigwangalla wazindua kambi ya upimaji wa afya bure

Muktasari:

Zoezi hilo la upimaji afya linaongozwa na madaktari bingwa kutoka China wanaoendesha kambi hiyo ya siku sita, iliyoanza Julai 24 na itafikia ukomo Julai 30.

Tabora. Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri amezindua rasmi kambi maalum ya upimaji afya bure kwa wananchi mbalimbali wilayani Nzega, ndani ya Hospitali ya Wilaya ya Nzega.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo leo Jumatano Julai 26, Mwanri ambaye alikuwa mgeni rasmi, amewapongeza waandaaji wa kambi hiyo na kueleza kuwa itasaidia kuboresha afya za wananchi.

“Wananchi wanahitaji afya njema, tunapongeza kambi hii kwani madaktari bingwa waliokuja hapa watatatua matatizo ya msingi kwenye afya zetu. Hivyo wananchi mjitokeze kwa wingi,” ameeleza Mwanri.

Mwanri amewapongeza madaktari bingwa kutoka China wanaoendesha kambi hiyo ya siku sita, iliyoanza rasmi Julai 24 na itamalizika Julai 30.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dk. Hamisi Kigwangalla ambaye pia ni Mbunge wa Nzega Vijijini, ameishukuru Serikali ya China kwa kufanikisha tukio hilo ikiwemo kutoa dawa za maralia kwani kwa msingi huo utasaidia kuokoa maisha ya wananchi wa Nzega.

“Tunapokea kwa mikono miwili msaada huu kutoka Serikali ya China hasa kupitia kwa balozi wake hapa nchini. Dawa hizi ni nyingi na hakika zitasaidia wananchi wote kuanzia wilaya ya Nzega na mkoa nzima wa Tabora, nawashukuru sana wananchi wanaojitokeza kupata huduma za matibabu kwenye kambi hii ya madaktari bingwa,” amesema Dk Kigwangalla.