Mwanzo mwisho kesi ya mauaji ya Msuya

Washitakiwa sita wa kesi ya mauaji ya mfanya biashara wa Madini ya Tanzanite Erasto Msuya,wakipanda magari ya Polisi kwa ajiri ya kurudishwa mahabusu katika Gereza Kuu la Karanga mkoani Kilimanjaro. Picha na Dionis Nyato

Muktasari:

  • Wakati upande wa mashtaka ukiishia mashahidi 32 kati ya 50 waliotarajia kuwaita, utetezi kwa upande wao uliita mashahidi nane na vielelezo vinne kupangua ushahidi wa mashitaka.

Moshi. Kesi ya mauaji ya kukusudia ya mfanyabiashara Erasto Msuya, imefikia ukingoni huku upande wa mashtaka ukiegemea mashahidi 32 na vielelezo 26 kujenga msingi wa kesi yao.

Wakati upande wa mashtaka ukiishia mashahidi 32 kati ya 50 waliotarajia kuwaita, utetezi kwa upande wao uliita mashahidi nane na vielelezo vinne kupangua ushahidi wa mashitaka.

Msuya aliyekuwa akimiliki vitega uchumi kadhaa jijini Arusha, aliuawa kwa kupigwa risasi na bunduki ya kivita ya Sub Machine Gun (SMG) Agosti 7, 2013 eneo la Mijohoroni wilayani Hai.

Katika eneo la tukio, kuliokotwa maganda ya risasi za SMG 22 huku gari ya marehemu aina ya Range Rover T800 CKF, bastola zake na simu zake mbili zikikutwa eneo la tukio.

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi, chini ya Jaji Salma Maghimbi aliyesikiliza kesi hiyo, ilipokea vielelezo kadhaa vya kesi hiyo ikiwamo bunduki ya SMG na maganda 25 ya risasi

Pia, ilipokea pikipiki mbili, moja aina King Lion T751 CKB na Toyo 316 CLG zinazodaiwa na mashahidi wa upande wa mashtaka, kuwa zilitumika kusafirisha wauaji.

Mbali na vielelezo hivyo, Mahakama ilipokea vielelezo vya nyaraka ambavyo ni maelezo ya onyo ya kukiri kosa ya washtakiwa watatu na maelezo ya ungamo yaliyotolewa kwa mlinzi wa amani.

Maelezo hayo ya onyo ni ya mshtakiwa wa kwanza, Sharifu Mohamed, mshtakiwa wa tatu, Mussa Mangu, mshtakiwa wa saba, Ally Majeshi na maelezo ya ungamo ni ya mshtakiwa Karim Kihundwa.

Pia, Mahakama ilipokea maelezo ya mashahidi watano wa upande wa mashtaka na kuyasoma mahakamani baada ya jitihada za upande wa mashtaka kuwapata kugonga mwamba.

Mtiririko wa tukio hilo lililovuta hisia za wananchi wengi katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara na linaloendelea kuvuta hisia hizo kwa sasa ulikuwa kama ifuatavyo:-

Agosti 7, 2013

Mfanyabiashara wa tajiri Mererani, Arusha na Moshi, bilionea Erasto Msuya aliuawa kwa kupigwa risasi sehemu mbalimbali za mwili wake katika eneo la Mjohoroni wilayani Hai.

Agosti 11, 2013

Polisi ilitangaza kukamatwa kwa washukiwa muhimu wakihusishwa katika mtandao wa wahalifu waliofanya mauaji hayo.

Agosti 21, 2013

Watuhumiwa watatu, Sharifu Mohamed, Shaibu Jumanne na Mussa Mangu walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi kujibu shtaka la kumuua kwa makusudi bilionea Msuya.

Septemba 16, 2013

Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro wakati huo, Robert Boaz alitangaza kukamatwa kwa watuhumiwa wanne zaidi kuhusiana na mauaji ya bilionea Msuya.

Watuhumiwa hao ni mfanyabiashara tajiri wa Mirerani na Arusha, Joseph Mwakipesile au Chussa, Sadick Mohamed, Karim Kihundwa na Jalila Said.

Septemba 18, 2013

Mfanyabiashara Mwakipesile au Chussa, Sadick, Karim na Jalila walifikishwa mahakamani kujibu shtaka la kumuua kwa makusudi bilionea Msuya.

Aprili 16, 2014

Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), alimfutia mashitaka mfanyabiashara Mwakipesile au Chussa akitumia kifungu Na 91 cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya Jinai (CPA) ya 2002.

Juni 10, 2014

Upande wa mashtaka ulifanya mchakato wa kuwasomea washtakiwa maelezo ya mashahidi 50 wa kesi hiyo na kutaja vielelezo vitakavyotumika wakati kesi hiyo.

Februari 10, 2015

Kwa mara ya kwanza washtakiwa walisomewa shtaka la mauaji ya kukusudia mbele ya Jaji Amaisario Munisi na wakakana kumuua Msuya.

Oktoba 5, 2015

Kesi ya mauaji ya kukusudia ya bilionea Msuya ilianza rasmi kusikilizwa na Jaji Salma Maghimbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha aliyeteuliwa kusikiliza kesi hiyo.

Ushahidi wa upande wa mashtaka

Ushahidi wa mashahidi wa mashtaka, ulidai kuwa njama za kumuua Msuya zilianza Julai 2013; watuhumiwa waliofanya mauaji hayo waliahidiwa kulipwa Sh17 milioni kila mmoja.

Ilidaiwa kortini kuwa katika kupanga mauaji hayo, simu mpya tano na laini tano zilisajiliwa kwa majina ya kimasai, kununuliwa kwa pikipiki mbili na kununuliwa kwa bunduki aina ya SMG.

Katika ushahidi huo, inadaiwa mshtakiwa wa saba, Ally Mussa Majeshi, ndiye aliyemvuta marehemu hadi eneo la tukio, akijifanya yeye na Karim walitaka kumuuzia madini ya Tanzanite.

Kulingana na maelezo ya ungamo ya mshtakiwa Karim na maelezo ya onyo ya kukiri kosa ya mshtakiwa wa saba, Majeshi, Karim ndiye anayedaiwa kumfyatulia risasi marehemu.

Katika ushahidi wake, Dk Paul Chaote aliyeufanyia uchunguzi mwili wa Msuya, alidai kuwa ulikuwa na majeraha 26 ya risasi yaliyosababisha mfumo wa damu na upumuaji kusimama.

Dk Chaote alidai kwa kuutazama kwa nje, mwili wa marehemu ulikuwa na majeraha madogo 13 na majeraha makubwa 13 yaliyosababishwa na risasi zilizoingia na kutokea upande wa pili.

Alidai baada ya kuupasua mwili wa marehemu, walikuta utumbo mwembamba umekatika huku risasi hizo zikiharibu figo, mishipa ya damu na bandama lilikuwa limepasuliwa kabisa.

Dk Chaote alidai mapafu yote mawili yaliharibiwa vibaya kwa risasi huku mishipa ya damu inayoingia kwenye mapafu, figo na bandama nayo ikiwa imechakazwa kwa risasi.

Katika ushahidi wao, mashahidi wote waliegemea katika ushahidi wa mazingira ambapo maofisa wa polisi walieleza namna washtakiwa walivyoshiriki tukio hilo na namna walivyowakamata.

Mshtakiwa wanne aachiwa huru

Mei 14, 2018 Jaji Maghimbi alisema baada ya kupitia ushahidi wa 32 wa mashtaka na vielelezo 26, amemuona mshtakiwa wa nne, Jalila hana kesi ya kujibu.

Alisema wakati washtakiwa wanafunguliwa mashtaka mwaka 2013, walikuwapo nane, lakini kuna mshtakiwa mmoja ambaye hata hivyo hakumtaja kwa jina aliachwa njiani.

Mfanyabiashara Mwakipesile alikuwa miongoni mwa washtakiwa lakini mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwa kutumia mamlakaka yake, alimfutia shtaka hilo Aprili 17,2014.

“Suala la ni kwanini aliachiwa njiani hilo ni suala la DPP. Kwa sasa hivi Mahakama inaona ushahidi unaonyesha washtakiwa sita mliobaki mna kesi ya kujibu na mtapaswa kujitetea,”alisema Jaji.

Utetezi wa washtakiwa ulivyokuwa

Katika utetezi wao, washtakiwa wote waliegemea ushahidi wa kutokuwapo eneo la tukio (alibi), wakidai kuliteswa na maofisa wa polisi wakiri kosa hilo na kuweka saini katika maelezo ya onyo.

Mshtakiwa wa kwanza, Sharifu Mohammed alidai siku ya tukio alikuwa katika machimbo ya madini ya dhahabu huko Londoni, Ikungi mkoani Singida na alirejea Arusha Agosti 11,2013.

Mshtakiwa wa pili, Shaibu Jumanne alidai siku ya mauaji,hakuwapo Arusha wala Kilimanjaro,alikuwa shambani Babati akivuna, kuanzia Julai 13 hadi Agosti 7,2013.

Mshtakiwa wa tatu, Mussa Mangu, alidai siku ya tukio alikuwa Singida akimuuguza baba yake na aliondoka Arusha Agosti 1,2013 kwa basi la Mohamed Classic na kurudi Arusha Agosti 7,2013.

Mshtakiwa wa tano, Karim Kihundwa alidai siku ya tukio alikuwa shambani kwake huko West Kilimanjaro akivuna karoti na alirejea nyumbani Bomang’ombe Agosti 10,2013.

Mshtakiwa wa sita, Sadik Jabir, alidai siku ya tukio alikuwa Jijini Dar es Salaam na baadaye alikwenda Kaliua Tabora na kukamatwa na polisi Septemba 13, 2013.

Mshtakiwa wa saba, Ally Majeshi alidai siku ya tukio alikuwa Magugu huko Babati akiwa katika mapumziko ya Fungate, baada ya kufunga ndoa Agosti 6, 2013 na Mwanaisha Juma.

Majumuisho ya mwisho Mei 24, 2018

Upande wa utetezi ulifunga kesi yao Ijumaa na uliiomba Mahakama chini ya Jaji Maghimbi, kufanya majumuisho ya mwisho huku upande wa mashtaka ukasema nao utafanya hivyo.

Jaji Maghimbi alikubali maombi hayo na kuahirisha kesi hiyo hadi Mei 24 mwaka huu na kwamba mawakili wa pande zote mbili watawasilisha majumuisho ya mwisho ya ushahidi wa pande zote.