Mwenge wa uhuru wazua jambo bungeni

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga amemzuia  mbunge wa Chadema kuuliza swali la nyongeza baada ya awali kudai mwenge unatumia gharama kubwa, kutaka uwekwe makumbusho ya Taifa, si kuzungushwa nchi nzima

Dodoma. Mwenge wa Uhuru leo Ijumaa Septemba 14, 2018 umeibua mzozo bungeni na kumlazimu mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga kumzuia mbunge wa Viti Maalum (Chadema),  Zubeda Sakuru kuuliza swali la nyongeza kuhusu jambo hilo.

Katika swali lake la  msingi  Zubeda ameihoji Serikali kama haioni umuhimu wa kuuweka  mwenge wa Uhuru katika makumbusho ya Taifa na kuzifuta sherehe zake kwa kuwa umekuwa ukitumia gharama kubwa.

Mwenge wa Uhuru ulianzishwa Desemba 9, 1961  kwa kupandishwa juu ya kilele cha Mlima Kilimanjaro siku ambayo Yanganyika ilipata uhuru wake kutika kwa Waingereza.

Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Antony Mavunde amesema Serikali haina nia kuuweka mwenge katika makumbusho kwa kuwa bado una faida kubwa kuliko hasara.

Mavunde amesema mwenge huo umekuwa ukiwakumbusha Watanzania falsafa nzito inayotoa taswira ya Taifa ambayo waasisi walitaka kuijenga katika Taifa lenye amani.

"Si kweli kwamba Mwenge unatumia fedha nyingi, mfano mwaka 2017 Serikali ilitenga Sh463milioni  kugharamia shughuli za mwenge lakini miradi iliyozinduliwa ni 1,512 yenye thamani ya sh 1.1 trilioni," amesema Mavunde.

Amesema kila mwaka mwenge huambatana na ujumbe muhimu wa kitaifa, kwamba mwaka 2017  ujumbe ulikuwa ni ‘shiriki kukuza uchumi wa viwanda kwa maendeleo ya nchi yetu’ na 2018 ujumbe ni ‘elimu ni ufunguo wa maisha, wekeza sasa kwa maendeleo ya Taifa’.

Baada ya majibu hayo, mbunge huyo alitaka kuuliza swali la nyongeza lakini Giga alimkatalia na kutoruhusu swali hilo kwa maelezo kuwa majibu yamejitosheleza jambo ambalo lilizua mvutano.