Mwenyekiti UVCCM kilombero akumbana na kero lukuki za wananchi

Muktasari:

Ni baada ya kufanya ziara katika kata mbili za Viwanja sitini na Michenga wilayani Kilombero.

Kilombero. Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Kilombero,  Muniph Utoto  jana Septemba 17,  2018 ametembelea kata za Viwanja sitini na Michenga na kupokea kero mbalimbali na kuahidi kuzifikisha katika uongozi wa juu wa chama hicho tawala.

Akizungumza na MCL Digital,  Utoto amesema baadhi ya kero hizo ni mikopo kwa vikundi vya vijana.

"Katika hata hizi mbili nimekuta changamoto ya uhaba wa zahanati. Zipo ila hazitoshi. Pia maji ni shida. Nimejionea na nitakwenda kuwasilisha mambo haya katika uongozi wa juu wa chama, " amesema.

"Lengo ni kuhakikisha chama kinatimiza ahadi zake ilizoahidi wakati wa uchaguzi."

Mwenyekiti huyo pia alikutana na baraza la vijana la kata hizo na kusikiliza changamoto zao.

Akiwa ameambatana  na wajumbe wake wa kamati ya utekelezaji, alikwenda nyumbani kwa  mwenyekiti wa zamani wa umoja huo, marehemu John Guninita aliyefariki dunia Septemba 13,  2018 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu. Guninita aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es Salaam,  atazikwa kesho mkoani Morogoro.