Mwenyekiti wa kijiji abanwa kuhusu mapato na matumizi

Mwenyekiti wa kijiji cha Matale wilayani Mvomero akijitetea mbele ya wananchi wa kijiji hicho waliotaka kufahamu mapato na matumizi ya fedha walizochanga kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa madarasa na nyumba ya walimu.

Muktasari:

Mwenyekiti wa kijiji Matale wilayani Mvomero amebanwa na wananchi wake wakitaka kupata taarifa ya mapato na matumizi ya ujenzi wa madarasa na nyumba ya walimu

Morogoro. Wananchi wa kijiji cha Matale wilayani Mvomero mkoa wa Morogoro wamemtaka mwenyekiti wa kijiji hicho, Khalifa Kibwana kuwasomea taarifa ya mapato na matumizi ya mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa na nyumba ya walimu wa Shule ya Msingi Matale.

Katika mkutano wa kijiji hicho uliofanyika leoulioandaliwa na asasi isiyo ya kiserikali ya Dira ya Maendeleo Tanzania (Dimata), wananchi hao walisema hawatafanya shughuli ya kujitolea tena mpaka watakapopata taarifa hiyo.

Mkazi wa kijiji hicho, Bakari Yahaya alisema tangu kuanza mradi wa ujenzi wa madarasa na nyumba za walimu miezi minne iliyopita, hawajawahi kuelezwa taarifa za fedha zilizopatikana licha ya kila mmoja wao kuchangia Sh5,000 zaidi ya miezi mitatu iliyopita.

Mwingine, Patrick Ndekelo alisema wananchi walijitolea kufyatua matofali kwa ajili ya ujenzi wa madarasa hayo lakini baada ya kuona hakuna taarifa yoyote  inayotolewa na uongozi wao waliamua kugomea kufanya shughuli za kujitolea.

“Wananchi tumesusa kuja hapa kujitolea kwa sababu viongozi wetu hawatupi taarifa ya mapato na matumizi, ndio maana wengi wetu wananong’ona mitaani bora mfadhili aondoke pamoja na kwamba mradi tunaupenda,” alisema Ndekelo.

Baada ya malalamiko hayo, Kibwana alisimama na kueleza tatizo ni wananchi kutohudhuria vikao pindi wanapoitwa na kuwaomba kumpa muda wa kukutana na mtendaji wa kijiji ili waandae majumuisho ya michango yote.

“Naomba niseme kwamba kwa muda mfupi mtapata majibu ya pamoja, ila naomba ushirikiano wenu wakati wa shughuli za maendeleo tujitokeze na kuzifanya wakati huo tukiendelea na uandaaji wa taarifa kwani tatizo lilikuwa kwa mtendaji wa kijiji ambaye alikuwa na udhuru,” alisema.

Aidha, mwenyekiti huyo aliwaomba wananchi kujitokeza kwa ajili ya kusomba matofali yaliyopo eneo la mtoni kwa ajili ya kuyafikisha eneo la shule ili ujenzi uendelee.

Akizungumza katika mkutano huo, katibu mtendaji Dimata, Salum Wamaywa alisema Serikali na mashirika yamekuwa yakitoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika shule za msingi lakini fedha hizo zimekuwa zikitumika visivyo na miradi kutomalizika kama ilivyolengwa.

 “Changamoto katika sekta ya elimu zipo nyingi ila Serikali imekuwa ikitumia lugha ya hamasa kwa wananchi lakini ufuatiliaji bado umekuwa mdogo, kinachotakiwa ni kuhakikisha inasimamia miradi inakamilika,” alisema Wamaywa.