Mwili mwingine wasuswa mochwari kwa siku 74

Ndugu wa marehemu Salum Kindamba, wakiwa nyumbani kwa kaka yake Kipawa jijini Dar es Salaam, juzi. Picha na Mpigapicha Wetu

Muktasari:

Familia ya Kindamba imegoma kuchukua mwili wa Salum katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kwa zaidi ya siku 10 ikidai kutoridhishwa na ripoti ya hospitali kuhusu chanzo cha kifo chake wanachokihusisha na kupigwa risasi na polisi eneo la Jet Rumo.

Mbeya/Dar. Siku moja baada ya gazeti hili kuripoti tukio la familia ya Kindamba ya jijini Dar es Salaam kususa kuchukua mochwari mwili wa ndugu yao, Salum Kindamba; familia ya Frank Kapange inayoishi jijini Mbeya imegoma kuchukua mwili wake.

Familia ya Kindamba imegoma kuchukua mwili wa Salum katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kwa zaidi ya siku 10 ikidai kutoridhishwa na ripoti ya hospitali kuhusu chanzo cha kifo chake wanachokihusisha na kupigwa risasi na polisi eneo la Jet Rumo.

Kwa upande wake, familia ya Frank ya jijini Mbeya imegoma kuchukua mwili wake kwa zaidi ya siku 74 ikinishikiza ufanyike uchunguzi kutokana na utata wa kifo chake wakiwatuhumu polisi kuhusika nacho.

Mwili wa Frank ambaye alikuwa mfanyabiashara Soko la Sido jijini Mbeya uko mochwari katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya tangu Juni 4, huku ndugu hao wakiwa wamefungua shauri katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, wakiiomba kutoa amri ya kufanyika uchunguzi wa kina wa kifo chake. Shauri hilo linatarajiwa kutajwa mahakamani hapo kesho.

Madai ya familia

Julius Kapange, msemaji wa familia ya Frank ambaye ni baba yake mkubwa, alisema kifo cha ndugu yao kina utata na wanaamini kwamba aliuawa akiwa mikononi mwa polisi.

Alisema wameamu kwenda mahakamani kutafuta haki ya kufanyika uchunguzi. “Kwa namna tulivyomuona ndugu yetu pale mochwari, tunaona kabisa aliuawa tu na polisi ndiyo tunaowatuhumu, kwani siku ya tukio alikuwa mikononi mwa polisi Kituo cha Mwanjelwa,” alisema.

“Tulimuona akiwa na majereha kichwani, shingo yake kama amenyongwa na tisheti yake ikiwa imechanika kifuani.”

Kapange alisema alipata taarifa kutoka kwa rafiki wa Frank ambaye siku tukio, Juni 4 alikutana naye katika Stendi ya Kabwe jijini hapa.

Akimnukuu rafiki huyo wa Frank, Kapange alisema waliachana kwa dakika chache, lakini aliporudi hakumkuta.

“Sasa aliposhuka pale chini (eneo walilokuwa) hakumkuta mwenzake (Frank), akaanza kumtafuta. Akakutana na mtu ambaye alimweleza kuwa yupo Kituo cha Polisi Mwanjelwa.”

Kapange alidai baada ya kupata taarifa kuwa alikuwa amekamatwa walikwenda polisi na kuulizia, lakini hawakupata ushirikiano na kulazimika kuondoka.

Alisema siku iliyofuata waliwahi Kituo cha Polisi Mwanjelwa na walipofika na kukosa ushirikiano kwa mara nyingine, walikwenda kituo kikuu cha polisi jijini hapa.

Alidai walipofika kituoni hapo walikutana na mama mmoja ambaye baada ya kumweleza mtu waliyekuwa wanamtafuta na kumuonyesha picha ya Frank, aliwaambia amefariki dunia na mwili wake umepelekwa mochwari.

Baada ya taarifa hizo, kwa mujibu wa Kapange, ndugu na marafiki walikwenda mochwari ya Hospitali ya Rufaa ya Mbeya na kuukuta mwili wake.

“Hata hivyo, sisi wanafamilia na marafiki wa Frank tuligoma kuuchukua na kuuzika mwili huo tukitaka kujua chanzo cha kifo chake,” alisema.

Baba huyo wa marehemu alisema wamekwishafungua jalada la kesi mahakamani wakiiomba iagize kufanyika kwa uchunguzi wa kifo hicho.

Akizungumzia suala hilo, Kamanda mpya wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei alisema lilitokea wakati yeye hayupo, hivyo halifahamu vizuri lakini akaahidi kulifuatilia.

Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Dk Petro Seme aliliambia Mwananchi kwamba, mwili wa marehemu bado upo mochwari tangu Juni 4 ulipopelekwa na polisi.

“Bado tumeuhifadhi mochwari na ni polisi case (suala la polisi), kwani hapa aliletwa na polisi, hivyo suala hili lipo chini ya polisi na tunasubiri taratibu zao,” alisema Dk Seme.

Aliongeza kuwa, “Lakini ndugu wa marehemu huyu walikuja kuutambua mwili baada ya siku tatu hivi baadaye.”

Matukio yanayofanana

Tukio jingine linalofanana na hayo ni lile la Mei, ambapo ndugu wa marehemu Salum Almasi walisusa kuchukua mwili wake wakidai ameuawa na polisi katika mazingira yenye utata eneo la makao makuu ya Idara ya Uhamiaji jijini Dar es Salaam.

Jingine ni lile la familia ya Mapunda ya Mtera wilayani Mpwapwa ambayo iligoma kuchukua mwili wa ndugu yao, Simon Mapunda (24), aliyedaiwa kuuawa na polisi wa kituo cha Mtera.