Mwili uliosuswa na ndugu kufikisha siku 90 mochwari

Muktasari:

Frank alifariki dunia Juni 4 na tangu wakati huo ndugu zake walisusa kuchukua mwili wakidai kuna utata kuhusu mazingira ya kifo chake.

Mbeya. Mwili wa marehemu Frank Kapande ambao familia yake imeususa kwa siku 76, utaendelea kubaki mochwari ya Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, baada ya Mahakama Hakimu Mkazi Mbeya kusema itatoa uamuzi wa mdogo Septemba 4.

Frank alifariki dunia Juni 4 na tangu wakati huo ndugu zake walisusa kuchukua mwili wakidai kuna utata kuhusu mazingira ya kifo chake, hivyo waliwasilisha ombi mahakamani wakiomba Mahakama itoe amri uchunguzi wa kina ufanyike wakilituhumu Jeshi la Polisi kuhusika.

Shauri hilo lilifunguliwa mahakamani Julai 30 na upande wa Jamhuri ukiongozwa na wakili Baraka Mgaya uliwasilisha pingamizi la awali ukidai maombi hayakufuata misingi ya kisheria.

Jamhuri ina hoja mbili za kupinga maombi hayo ikidai kiapo kilichowasilishwa kinaonyesha wakili wa walalamikaji, Moris Mwamwenda ndiye aliyeapa badala ya mwombaji Julius Kapange.

Hoja nyingine ni kiapo hicho kutoeleza bayana kimechukuliwa kutoka wapi, hivyo Jamhuri inaiomba Mahakama kutupilia mbali ombi hilo.

Waombaji wameshindwa kuwasilisha majibu ya hoja za pingamizi hilo kwa muda uliopangwa ambapo hadi jana hawakuwa wamewasilishwa.

Septemba 4, Mahakama imepanga kutoa uamuzi wa pingamizi hilo ikiwa na maana mwili wa marehemu utakuwa unatimiza siku 90 tangu alipofariki dunia ukiwa haujazikwa.

Wakili wa Serikali, Mgaya alisema mahakamani jana kuwa, Agosti 15 alipokea barua kutoka kwa wakili Mwamwenda akiomba kuongezewa muda wa kujibu pingamizi, lakini hadi jana hakuwa amefanya hivyo, hakuwapo mahakamani na simu yake haikupatikana.

Aliiomba Mahakama iendelee kuandika uamuzi mdogo kwa kuwa Jamhuri ilishawasilisha hoja zake kwa maandishi.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Michael Mteite alimuuliza muombaji katika shauri hilo, Kapange ambaye ni baba mkubwa na marehemu Frank alipo wakili wake. Kapange alisema hana taarifa za kutoonekana kwa wakili huyo.

Hakimu Mteite alimweleza mwombaji kwamba Julai 23, upande wa Jamhuri uliwasilisha mahakamani pingamizi dhidi ya maombi yake na walitakiwa kuyawasilisha kwa maandishi, jambo walilolitekeleza Julai 30.

Alimweleza Kapange kuwa wakili wake alitakiwa kujibu hoja hizo ndani ya siku 14, lakini hadi jana asubuhi hakuwa amefanya hivyo.

“Ninyi na wakili wenu hamjawasilisha hoja zenu ili mahakama iweze kutoa uamuzi mdogo, wala wakili mwenyewe hayupo mahakamani na hajatoa taarifa zozote iwe kwa mahakama hii au kwa wakili mwenzake,” alisema Hakimu Mteite. “Sasa kama anavyosema wakili wa Serikali hapa kwamba hampo serious (makini) na suala hili, naungana naye maana kama ni muda wa nyongeza aliouomba alipewa.”

Alisema suala la kutofika kwa wakili wa utetezi si kosa la Jamhuri, bali ni la wakili mwenyewe, hivyo atatoa uamuzi mdogo wa hoja za upande wa Jamhuri Septemba 4.

Soma Zaidi: