Mzee Majuto atoboa siri ya alichozungumza na Kikwete

Muktasari:

Kwa mujibu wa Majuto mpaka sasa ana shamba lenye ukubwa wa eka tano 

Dar es Salaam. Siku chache baada ya kusambaa kwa picha zikimuonyesha mchekeshaji Amri Athumani maarufu Mzee Majuto akizungumza na Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, leo Alhamisi Aprili 5, 2018 ameeleza walichoteta.

Picha hiyo ilipigwa wakati Kikwete alipokuwa akiondoka ukumbi wa Mlimani City kulikokuwa kukifanyika  hafla ya utoaji  tuzo za filamu za SZIFF, zilizoandaliwa na kituo cha televisheni cha  Azam kupitia chaneli yake ya Sinema Zetu.

Akizungumza na MCL Digital leo Mzee Majuto amesema aliahidiwa na Kikwete kupewa trekta la kulimia.

Katika maelezo yake, msanii huyu amesema  trekta hilo aliahidiwa na rais huyo mstaafu  wakati wa sherehe iliyowakusanya wasanii wa fani mbalimbali za kumuaga mwishoni mwa mwaka 2015.

“Nakumbuka mara ya kwanza kuomba trekta hili kwa Rais Kikwete ilikuwa nilipohojiwa katika kipindi cha Mikasi kilichokuwa kikirushwa na kituo cha EATV, lakini jambo hili pia nilimkumbushia wakati alipokutana na wasanii pale Mlimani City Jijini Dar es Salaam katika sherehe za kumuaga,” amesema Majuto.

“Nilipokutana naye tena kwenye tuzo nikaona si vibaya nikamkumbushia kwa kuwa najua ni mtu mwenye mambo mengi na watu wengi wanamfikia kwa ajili ya kupata msaada.”

Kwa mujibu wa Majuto mpaka sasa ana shamba lenye ukubwa wa eka tano na kwa kuwa amedhamiria kuachana na sanaa tangu aliporudi kutoka kuhiji, atawekeza nguvu zake zaidi katika kilimo.