NMB yatenga Sh500 bilioni viwanda vya kilimo, mifugo

Mkuu wa kitengo cha wateja wakubwa na Serikali wa NMB, Filbert Mponzi

Muktasari:

  • Imetenda fedha hizo kwa ajili ya kuwakopesha wajasiriamali wenye viwanda vya ngozi na wanaosindika mazao ya kilimo.

Dodoma. Kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika kujenga uchumi imara, Benki ya NMB imetanga Sh500 bilioni kwa ajili ya wajasiriamali wa sekta ya kilimo na ngozi.

Mkuu wa kitengo cha wateja wakubwa na Serikali wa NMB, Filbert Mponzi leo amesema fedha hizo zitakopeshwa kwa miaka mitano ili kuwapa fursa wananchi kushiriki kuujenga uchumi wao.

“Uchumi wa viwanda unategemea sana sekta ya kilimo na mifugo, hivyo NMB itaendelea kuwa mstari wa mbele kuwasaidia wajasiriamali wadogo kupata mikopo nafuu na rafiki ili kuimarisha miradi yao,” alisema Mponzi.

Alisema hayo kwenye mkutano mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) na kubainisha kuwa benki hiyo imekuwa karibu na Serikali katika utekelezaji wa masuala mengi ikiwamo kuinua jamii kiuchumi.

Kwa miaka miwili iliyopita, ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaonyesha kupungua kwa mikopo ya benki za biashara kwenda sekta binafsi kulikochangiwa na kuongezeka kwa mikopo isiyolipika kulikochangia kushusha faida ya taasisi nyingi za fedha nchini.

NMB ndiye mdhamini wa mikutano mikuu ya ALAT kwa miaka sita mfululizo. Mwaka huu benki hiyo imetoa Sh100 milioni kufanikisha mkutano huo.

Baada ya kukopesha zaidi ya Sh280 bilioni kwa wakulima na wasindikaji wa mazao nchini kwa miaka miwili iliyopita, Mponzi alisema wameongeza bajeti ili kuwanufaisha wananchi wengi zaidi.

Mchumi na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Mutahyoba Baisi alisema NMB imeonyesha mfano jambo linalopaswa kuigwa na taasisi nyingine za fedha kufanikisha malengo ya nchi.

“Uchumi wa viwanda unahitaji ushiriki wa taasisi za fedha. NMB ni benki kubwa inayopaswa kuonyesha njia kwa wengine. Ni fedha nyingi kwa kuanzia lakini kulingana na mahitaji yaliyopo hazitoshi,” alisema Dk Baisi.

Takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) zinaonyesha kuwa, zaidi ya Sh32 trilioni zinahitajika kuweza kuinua uchumi kutoka nchi inayoendelea kwenda ya uchumi wa kati.

Meneja wa NMB Kanda ya Kati, Msolo Mlozi alisema wamejipanga kusaidia maendeleo ya sekta mbalimbali hususan kipindi hiki Serikali ilipohamishia makao makuu jijini Dodoma.