Wednesday, February 14, 2018

VIDEO-NEC, Chadema na Polisi patashika Kinondoni

By Waandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Wakati wagombea ubunge wa majimbo ya Kinondoni na Siha wakiendelea kujinadi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imejibu malalamiko matano yaliyotolewa na Chadema.

Pia, Nec imevitaka vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi huo kuzingatia maadili ya uchaguzi, sheria na kanuni nyingine za nchi.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Nec, Ramadhani Kailima alijibu malalamiko hayo jana huku Chadema ikiibuka na malalamiko mengine, safari hii yakilihusu Jeshi la Polisi kuvamia ofisi zake za Kanda ya Pwani zilizopo Magomeni jijini Dar es Salaam na kupiga mabomu ya machozi kisha kuwakamata wanachama kadhaa.

Katika taarifa yake ya jana, Nec iliyataja malalamiko hayo matano ya Chadema dhidi yake na watendaji iliowateua kusimamia uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni ambao kama ilivyo Siha utafanyika Jumamosi.

“Kwa nyakati tofauti kati ya Februari 6 na 7, kupitia vyombo vya habari Chadema walitoa malalamiko dhidi ya Nec na watendaji wake walioteuliwa kusimamia uchaguzi mdogo katika Jimbo la Kinondoni,” ilieleza taarifa hiyo.

Malalamiko ya Chadema

Mosi, Chadema iliiandikia barua tume hiyo kuhusu wakuu wa wilaya kushiriki mikutano ya kampeni kuwanadi wagombea wa CCM na Nec kushindwa kuchukua hatua.

Pili, Nec ilidaiwa kuhamisha vituo vya kupiga kura 46 katika kata tatu za Kigogo, Mwananyamala na Kijitonyama bila kukishirikisha chama hicho.

Tatu, Chadema ilidai msimamizi wa uchaguzi alitoa maamuzi dhidi ya chama hicho kwenye kamati ya maadili kwa uonevu.

Nne, Chadema ilidai kuadhibiwa katika kamati hiyo kwa makosa wanayotuhumiwa kutendwa na Chadema na kuwa makosa hayo ni ya kijinai na yalipaswa kushughulikwa kijinai na sio kuipa adhabu Chadema na kwamba kikao hicho kiliendeshwa na asiyepaswa kuwa mwenyekiti wa kamati.

Tano, ni malalamiko ya Chadema dhidi ya wakuu wa wilaya kushiriki kampeni za uchaguzi waliyoyapeleka kwenye kamati za maadili kutotendewa haki kwa sababu wenyeviti wa kamati hizo ni makatibu tawala wa wilaya.

Majibu ya Nec

Katika majibu yake kuhusu hoja ya kwanza, Nec imesema, “Hadi kufikia leo Februari 13, 2018 (jana) hatujapokea barua yoyote kutoka Chadema.”

Kuhusu hoja ya kubadili vituo katika kata tatu ilieleza, “Hilo limefanyika kwa kuzingatia matakwa ya kanuni ya 21 ya kanuni za uboreshaji daftari la kudumu la wapiga kura za mwaka 2008 kama ilivyorekebishwa mwaka 2014 ikisomwa pamoja na kipengele cha 9.2(c) ya kitabu cha maelekezo cha wasimamizi wa uchaguzi ya mwaka 2015.”

Katika lalamiko la tatu la Chadema, Nec ilisema sheria, kanuni na maadili ya uchaguzi hayampi mamlaka msimamizi wa uchaguzi kutoa maamuzi kwenye kamati ya maadili.

“Tulitegemea Chadema walipoona hawakuridhika na maamuzi ya kamati ya maadili ngazi ya jimbo kufuata taratibu za kuwasilisha rufaa yao kwenye mamlaka husika kwa muda ulioanishwa badala ya kulalamika kwenye vyombo vya habari,” ilieleza.

Kuhusu kamati za maadili kutotenda haki kwa kuwa wenyeviti wa kamati hizo ni makatibu tawala wa wilaya, Nec ilisema hakuna kifungu chochote cha sheria au kanuni za uchaguzi au kipengele chochote cha maadili ya uchaguzi kinachosema katibu tawala wa wilaya ni mwenyekiti wa kamati ya maadili ya uchaguzi.

Kuvamiwa ofisi za Chadema

Akizungumza kuhusu kuvamiwa kwa ofisi za Chadema, mkurugenzi wa operesheni na mafunzo wa chama hicho, Benson Kigaila alisema juzi saa 12 jioni wakiwa kwenye kikao cha majumuisho katika ofisi hizo, walivamiwa na Polisi waliowakamata baadhi ya wanachama.

“Tukiwa ndani tunafanya kikao cha majumuisho ghafla polisi walivamia wakiwa pamoja na vijana wa CCM na kuanza kupiga mabomu na kuchukua vijana wetu,”alisema Kigaila.

Alisema wanachama wa Chadema wakiwa nje ya ofisi hiyo walimkamata mwanachama wa CCM akiwa anaandikisha shahada za kupigia kura jirani na ofisi hiyo, pamoja na kuchukua nakala za vitambulisho. Alibainisha kuwa baadhi ya viongozi waliokamatwa ni mkurugenzi wa Rasilimali Watu, Aron Mashuve; mwenyekiti wa Jimbo la Kawe, Powel Mfinanga; diwani wa Kibamba, Ernest Mgawe na wanachama wa kawaida akiwamo Japhari Namo.

Wengine ni Lilian Kimei, Muhamed Musa, Mputa Almasi, Ramadhan Mohamed, Frank Sylus, Aisha Musa, Christina Mpya, Ladslaus Focus, Ally Ashraf, Michael Sale, Casim Chepe, Abdalah Mkopi, Emanuel Mpanda na Gadner James.

Kigaila pia aligusia mawakala wa Chadema waliokula kiapo siku tatu zilizopita kwa ahadi ya kupewa viapo vyao siku iliyofuata, “Mpaka sasa bado hawajapewa viapo vyao. Tunapenda kumwambia mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni ikifika leo jioni (jana) hatujapewa viapo tutawambia mawakala wetu wakavidai.”

Naye Katibu wa Chadema mkoa wa Kinondoni, Henry Kileo alisema kuzuia viapo vya mawakala kwa nia ya kushinda itakuwa ngumu, kama havitatoka uchaguzi huo hautafanyika.

Polisi wajibu

Akizungumza na Mwananchi kuhusu tukio hilo Kamanda wa Polisi Kinondoni, Jumanne Muliro alisema tangu kuanza kwa kampeni polisi wamekuwa na utaratibu wa kufanya doria maeneo mbalimbali kuhakikisha usalama.

Muliro alisema hakuna taarifa ya Polisi kuvamia ofisi ya Chadema kama zinazosambaa ila walipita maeneo ya ofisi hizo ambazo ziko karibu na barabara kubwa.

“Watu wasitafsiri vibaya, Polisi tuna utaratibu wa kufanya doria tangu kampeni zimeanza na tunapita katika ofisi mbalimbali za chama. Hatujavamia ofisi yoyote wasichukulie jambo hili kisiasa,” alisema Muliro.

Wagombea

Mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM, Maulid Mtulia akiwa Kinondoni Shamba alisema mamlaka yake yalikuwa ni kujiuzulu ubunge lakini hakuwa na uwezo wa kujiteua kuwa mgombea ubunge.

‘“Leo nina miezi mitatu akaunti zangu zipo ziro hazisomi kama usaliti nimejisaliti mwenyewe sijamsaliti mtu,’’ alisema Mtulia

Alisema wazee wa Kamati Kuu (CCM) kwa hekima walimteua kuwa mgombea, pamoja na bahati nasibu aliyoifanya kwa wana- Kinondoni kwa kutokujua kitakachotokea siku iliyofuata.

‘’Nilikusudia kuleta mabadiliko makubwa ya makazi katika Jimbo la Kinondoni, hivyo uteuzi huu utafanikisha kutimiza ndoto zangu’’ alisema.

Mgombea ubunge wa Chadema Jimbo la Kinondoni, Salum Mwalimu akiwa Kata ya Mzimuni jana aliwataka wananchi jimbo hilo wamchague ili akashike nafasi ya mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Tundu Lissu mpaka atakaporudi kutoka kwenye matibabu Ubelgiji.

Alisema amejiandaa kupigwa risasi kwa ajili ya kupigania maslahi ya wananchi wa Kinondoni wanaoonewa kwa kubomolewa nyumba zao bila fidia.

Mgombea ubunge katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Siha, Dk Godwin Mollel (CCM), alisema akichaguliwa tena kuliongoza jimbo hilo, atawatafutia wakulima maeneo ya kilimo pamoja na kuhakikisha wanapata pembejeo.

Mbali na kilimo, pia alisema atahakikisha wananchi wanajengewa matenki ya maji safi na kusambaziwa katika maeneo yao, pamoja na kufikisha umeme katika vijiji ambavyo havijafikiwa.

Akiwa katika Kijiji cha Kandashi Kata ya Karansi, Dk Mollel alisema kijiji hicho kinakabiliwa na tatizo kubwa la upungufu wa maji, hivyo akichaguliwa tena atahakikisha anasambaza maji katika vijiji vyote na kuwaondolea wananchi adha wanazokumbana nazo kwa sasa.

“Natambua hapa mna tatizo la maji, naombeni mnipe nafasi, ili nishirikiane na Serikali kuhakikisha mnapata huduma ya maji safi na salama tena ya kutosha kama ilivyo maeneo mengine, pia nitahakikisha wakulima wanapata maeneo ya kilimo na pembejeo,” alisema Dk Mollel.

Mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia CUF Tumsifueli Mwanri, alisema kama atachaguliwa kuongoza jimbo hilo atajenga josho na mabirika ya mifugo kupata maji

Alisema changamoto zinazowakabili wafugaji wengi katika jimbo hilo ni sehemu ya mifugo kupata sehemu ya kupata maji.

Imeandikwa na Flora Temba, Bahati Chume (Moshi), James Magai, Tausi Ally, Kalunde Jamal, Fortune Francis, Jackline Masinde na Pamela Chilongola(Dar)

-->