Tuesday, February 13, 2018

NEC yajibu hoja tano za Chadema

 

By Kalunde Jamal, Mwananchi kjamal@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imejibu malalamiko matano yaliyotolewa dhidi yake na Chadema, huku ikivitaka vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi wa ubunge katika Jimbo la Kinondoni kuzingatia maadili ya uchaguzi, sheria na kanuni nyingine za nchi.

Kupitia taarifa yake iliyotolewa leo Februari 13, 2018 na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Kailima Ramadhani, imeeleza malalamiko hayo ya Chadema na kuyatolewa majibu ya kina.

“Kwa nyakati tofauti kati ya Februari 6 na 7, kupitia vyombo vya habari Chadema walitoa malalamiko dhidi ya NEC na watendaji wake walioteuliwa kusimamia uchaguzi mdogo katika Jimbo la Kinondoni,” inaeleza taarifa hiyo.

Malalamiko ya Chadema

Mosi, Chadema kuiandikia barua tume hiyo kuhusu wakuu wa wilaya kushiriki mikutano ya kampeni za kuwanadi wagombea wa CCM na NEC kushindwa kuchukua hatua.

Pili,  NEC kudaiwa kuhamisha vituo vya kupigia kura 46 katika kata tatu za Kigogo, Mwananyamala na Kijitonyama bila kukishirikisha chama hicho.

Tatu, Chadema inadai kuwa msimamizi wa uchaguzi kutoa uamuzi dhidi ya chama hicho kwenye kamati ya maadili kwa uonevu.

Nne ni Chadema kuadhibiwa katika kamati hiyo kwa makosa wanayotuhumiwa kutenda na kuwa, makosa hayo ni ya kijinai na yalipaswa kushughulikwia kijinai na sio kuipa adhabu Chadema na kwamba kikao hicho kiliendeshwa na asiyepaswa kuwa mwenyekiti wa kamati.

Tano, ni malalamiko ya Chadema dhidi ya wakuu wa wilaya kushiriki kampeni za uchaguzi waliyoyapeleka kwenye kamati za maadili kutotendewa haki kwa sababu wenyeviti wa kamati hizo ni makatibu tawala wa wilaya.

 

Majibu ya NEC

Katika majibu yake NEC imeanza kwa kujibu hoja ya kwanza ya Chadema, “Hadi kufikia leo Februari 13, 2018 hatujapokea barua yoyote kutoka Chadema.”

Kuhusu hoja ya kubadili vituo katika kata tatu imesema, “Hilo limefanyika kwa kuzingatia matakwa ya kanuni ya 21 ya kanuni za uboreshaji daftari la kudumu la wapiga kura za mwaka 2008 kama ilivyorekebishwa mwaka 2014 ikisomwa pamoja na kipengele cha 9.2(c) cha kitabu cha maelekezo cha wasimamizi wa uchaguzi ya mwaka 2015.”

Katika lalamiko la tatu la Chadema, NEC imesema sheria, kanuni na maadili ya uchaguzi hayampi mamlaka msimamizi wa uchaguzi kutoa uamuzi kwenye kamati ya maadili.

“Sheria, kanuni na maadili ya uchaguzi hayampi mamlaka msimamizi wa uchaguzi kutoa maamuzi kwenye kamati ya maadili,” inaeleza taarifa hiyo.

“Msimamizi wa uchaguzi ni mwenyekiti wa kikao cha maadili tu, kwamba maamuzi hufanywa na kamati ya maadili na sio mwenyekiti wa kamati. Hivyo, si sahihi kusema kuwa maamuzi ya kamati ya maadili yalifanywa na msimamizi wa uchaguzi ambaye ni mwenyekiti wa kamati husika,” inaeleza.

Inafafanua kuwa kamati ya maadili Kinondoni ina wajumbe 12 kutoka vyama 12 vinavyoshiriki uchaguzi na Kasmiri Mabina ni mjumbe wa kamati ya maadili kutoka Chadema.

”Kama maamuzi yametolewa kwa upendeleo alikuwepo mjumbe wao na si msimamizi wa uchaguzi,” inasema NEC.

Kuhusu kuadhibiwa katika kwenye kamati ya maadili kwa makosa yanayotuhumiwa kutendwa na mwanachama wa Chadema, NEC imesema chama cha siasa au mgombea ambaye hakuridhika na uamuzi uliotolewa na kamati ya maadili katika ngazi husikia, hufuata taratibu zilizoanishwa kwenye maadili ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani ya mwaka 2015 ili kupata haki yake kwa kuwasilisha rufaa kwenye mamlaka husika.

“Tulitegema Chadema walipoona hawakuridhika na maamuzi ya kamati ya maadili ngazi ya jimbo kufuata taratibu za kuwasilisha rufaa yao kwenye mamlaka husika kwa muda ulioanishwa badala ya kulalamika kwenye vyombo vya habari,” inaeleza.

Kuhusu kamati za maadili kutotenda haki na kuwa wenyeviti wa kamati hizo ni makatibu tawala wa wilaya, NEC imesema hakuna kifungu chochote cha sheria au kanuni  za uchaguzi ama kipengele cha maadili ya uchaguzi kinachosema katibu tawala wa wilaya ni mwenyekiti wa kamati ya maadili ya uchaguzi.

 

 


-->