NMB yaja na huduma mpya kwa ajili ya wajasiriamali

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Ineke Bussemaker (kulia) akizungumza na waandishi wa habari, hawapo pichani. Picha na Maktaba 

Muktasari:

Mjarisiamali atakayefungua akaunti hiyo atakuwa kwenye nafasi ya kupata mkopo kuanzia Sh 50,0000 hadi Sh30 milioni ambao riba yake itakuwa asilimia 2 kwa mwezi.

Dar es Salaam. Benki ya NMB imezindua huduma mpya kwa ajili ya kuwainua wajasiriamali wadogo wakiwemo mamalishe, madereva bodaboda na machinga.

Huduma hiyo inayofahamika kama NMB Fanikiwa Account itawawezesha wajasiriamali wadogo kutunza fedha zao na kupata mikopo kulingana na mzunguko wa biashara.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo Mkurugenzi wa NMB, Ineke Bussermaker amesema akaunti hiyo imekuja kuwakomboa wajasiriamali wenye vipato vidogo kabisa.

Bussermaker amesema  kupitia huduma hiyo wajasiriamali wadogo watapa fursa ya kuingia kwenye mfumo rasmi na kutambulika kiasi cha kukidhi vigezo vya kupata mikopo.

"Tunamaanisha kipato kidogo hapa mjasiriamali mwenye Sh 20000 anaweza kufungua akaunti na kila mwezi akawa anajiwekea kuanzia Sh 2000.Hiki ni kiwango kidogo zaidi kuwahi kutokea ikilinganishwa na akaunti nyingine,"amesema Bussemaker.

Kwa upande wake Mkuu wa huduma za benki wa NMB, James Meitaron amesema huduma hiyo itamwezesha mjasiriamali kuunganishwa na klabu za wafanyabiashara zilizo chini ya benki hiyo.

"Kupitia jukwaa hilo wajasiriamali wanabadilishana mawazo na kupeana ujuzi wa stadi mbali za biashara wenzao,"amesema.