Nacte yafungia udahili vyuo 163 kwa kukosa sifa

Mkuu wa kitengo cha udahili Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi  NACTE, Twaha  Twaha akizungumza na wandishi wa Habari jijiniDar es Salaam jana kuhusu udahili wa wanafunzi Kwenye kozi mbalimbali. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji ,Udhibiti na Tathimini, Dk Annastella  Sigwejo. Picha na Omar Fungo

Muktasari:

Kwa mujibu wa Nacte, kuna idadi ya vyuo 580, lakini vilivyofanyiwa uhakiki ni 429.

Dar es Salaam. Karibu nusu ya vyuo vilivyofanyiwa uhakiki na Baraza la Taifa la Elimu na Ufundi (Nacte), vimebainika kukosa sifa ya kudahili wanafunzi.

Baada ya uhakiki huo, imebainika kuwa vyuo hivyo vya ngazi ya shahada na astashahada, havina walimu wenye sifa, uwiano kati ya walimu na wanafunzi na miundombinu ikiwamo madarasa.

Kwa mujibu wa Nacte, kuna idadi ya vyuo 580, lakini vilivyofanyiwa uhakiki ni 429.

Kati ya hivyo, 163 vilibainika kuwa na mapungufu hayo na ni 266 tu ndivyo vilivyoonekana kuwa safi na vikaruhusiwa kudahili wanafunzi.

Lakini wamepewa muda mpaka mwishoni mwa Machi kurekebisha kasoro hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Nacte, Dk Annastella Sigwejo alisema walifanya uhakiki kwa jumla ya vyuo 459, kati ya hivyo, 266 ndivyo vimekidhi vigezo vya kutoa elimu kwa kiwango kinachotakiwa.

“Kutokana na hali hiyo, hivyo ndivyo vinaruhusiwa kudahili wanafunzi kwa ajili ya kozi mbalimbali ngazi ya astashahada na stashahada kwa muhula wa udahili wa Machi na Aprili mwaka huu,”alisema.

Alisema licha ya kwamba vyuo vilivyosajiliwa vipo 580 waliamua kujiridhisha kwa kuvifanyia uhakiki na walifanya kwa vyuo 459.

Nacte wanawashauri wanafunzi kuhakikisha wanajiridhisha wanapoomba kujiunga kwenye vyuo vilivyokidhi vigezo.

Mkuu wa Kitengo cha Udahili, Twaha Twaha alisisitiza kuwa majina ya vyuo vilivyoruhusiwa kudahili yamewekwa kwenye tovuti ya Nacte.

“Hivyo Nacte inashauri waombaji wa udahili kujiridhisha kwa kuangalia hiyo orodha iwapo chuo anachokitaka kinaruhusiwa kudahili,”alisema Twaha

Kaimu mkurugenzi mkuu wa Veta, Dk Bwire Ndazi akizungumzia kuhusu hatua hiyo alisema vyuo vinavyotoa elimu bila kuzingatia mwongozo vinapaswa kupewa adhabu ili kukomesha tabia hizo, ambazo zinachangia kurudisha nyuma maendeleo ya taifa.

“Tunapaswa kusimamia mwongozo wa elimu ile ya juu ina mwongozo wake upo, vivyo hivyo elimu ya kati na ufundi, ikiwamo inayotolewa na vyuo vya Veta ili kuhakikisha mwanafunzi anayehitimu amefuzu vyema kile anachotakiwa kusomea,” alisema Dk Bwire.

Alisisitiza kuwa ni jukumu la mzazi au mlezi kudadisi taarifa sahihi za chuo husika, hata kupitia tovuti atapata taarifa zinazomwezesha kuwa na uhakika wa uhalali wa masomo yanayotolewa hapo.

Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Omari Mbura alisisitiza chuo kujisajili kabla ya kutoa elimu kwa kuwa hiyo ni hatua mojawapo ya kutimiza vigezo vya uhakika wa elimu inayotolewa.

“Nacte inapaswa kuvitaja vyuo vyote vinavyobainika kutosajiliwa, hii itakuwa ni hatua nzuri ya kuwashtua wazazi na kuwafanya wawe makini,” alisema.

Dk Mbura, ambaye pia ni miongozi mwa wakaguzi wa vyuo anaeleza kuwa kuna vyuo vyenye mazingira mabaya hayafai kwa elimu, ikiwamo kukosa vifaa vya kufundishia.

“Ili mwanafunzi anayehitimu mafunzo awe bora ni lazima awe amefundishwa kwenye mazingira mazuri na walimu wenye uelewa mzuri kwa fani husika, “ alisema .

Katibu mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Leornard Akwilapo akizungumzia hatua hiyo iliyotangazwa na Nacte alieleza kwa kifupi kuwa ingawa bado hajaipata taarifa, lakini taasisi hiyo inatekeleza sera zinazosimamiwa na wizara hiyo.