Ndege kutumika kusaka wavuvi haramu

Dar es Salaam. Wakati vitendo vya uvuvi haramu vikiwa vimeshamiri katika maziwa na Bahari ya Hindi, Serikali imezindua mkakati unaolenga kuvitokomeza kwa kuanzisha operesheni inayotumia ndege maalumu kufanya doria katika eneo la bahari kuu.

Akizungumza wakati wa kuzindua operesheni hiyo baada ya ndege kutoka Mauritius kutua nchini kwa mara ya kwanza kufanya doria eneo la majini, Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega alisema lengo ni kudhibiti uvuvi haramu.

“Tunaruhusu ndege ya doria leo, (jana) ili kuongeza nguvu za kudhibiti uvuvi haramu, tulianza kwa njia ya bahari na sasa ni kwa anga. Changamoto ya uvuvi haramu ni kubwa, mtu anapiga bomu kwenye matumbawe, anafanya uharibifu ambao kutengeneza tena inachukua zaidi ya miaka 100, huku yeye akiharibu kwa dakika tano, ” alisema Ulega.

Alifafanua kuwa uharibifu huo unachangia umaskini kwa wavuvi wengi kwa sababu siyo rahisi kupata samaki karibu na kulazimika kwenda mbali ambako siyo rahisi kufika bila kuwa na vyombo maalumu.

Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Hamad Rashid Mohammed alisema atashauriana na marais wa pande zote mbili kuangalia namna ya kurudisha Shirika la Uvuvi Tanzania (Tafico) na Shirika la Uvuvi Zanzibar (Zafico).

Alisema mashirika hayo yakifanya kazi kwa kushirikiana, wananchi watapata fursa ya kufurahia matunda yatokanayo na utajiri uliomo baharini.

“Katika mwendelezo wa kupambana na uvuvi haramu na kulinda Bahari ya Hindi, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilifanya mazungumzo ya kuingia ubia na Serikali ya China na tayari kuna meli 10 zinafanya doria.

“Serikali pia, imeagiza boti 500 watakazopewa wavuvi ili wazitumie kuvua kisasa,” alisema.

Katibu Mkuu (Uvuvi), Dk Yohana Budeba alisema ndege hiyo itafanya doria ya anga eneo la bahari kuu kwa siku nne.

Kaimu mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu, Hosea Mbilinyi alisema ndege hiyo ina uwezo wa kupiga picha na kueleza kinachoendelea.