Ndege yakwamisha kesi ya Halima Mdee

Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee.

Muktasari:

  • Kesi ya kutoa lugha chafu dhidi ya Rais John Magufuli inayomkabili mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee imekwama kusikilizwa katika Mahakama  ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya mshtakiwa huyo kushindwa kufika mahakamani

Dar es Salaam. Kesi ya kutoa lugha chafu dhidi ya Rais John Magufuli inayomkabili mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee imekwama kusikilizwa katika Mahakama  ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya mshtakiwa huyo kushindwa kufika mahakamani.

Mdee ameshindwa kufika mahakamani baada ya ndege aliyopanga kusafiri nayo hadi jijini Dar es Salaam jana Jumapili Oktoba 21, 2018 akitokea mkoani Mwanza kuahirisha safari.

Wakili wa utetezi, Peter Kibatala ameeleza hayo leo Jumatatu Oktoba 22, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakati shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.

"Kutokana na mteja wangu kushindwa kufika mahakamani hapa  amekuja mdhamini wake,  Phares Rutomo ambaye ataeleza kwa undani sababu za Halima kushindwa kufika mahakamani,” amesema Kibatala.

Kibatala  baada ya kueleza hayo Hakimu Simba alimuuliza Rutomo sababu za mshtakiwa huyo kushindwa kufika mahakamani.

"Nimepewa taarifa na Mdee kuwa ndege aliyotarajia kurudi nayo jana jioni (Jumapili) kutoka Mwanza kuja Dar es Salaam imeahirisha safari hivyo ameshindwa kurudi Dar es Salaam kutokana na tatizo hilo,” amesema.

“Halima alienda Mwanza kikazi tangu Jumamosi na alitarajiwa kurudi Jumapili jioni ili leo aweze kuhudhuria kesi yake.”

Hakimu Simba baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 20, 2018 kesi hiyo itakapoendelea na ushahidi.

Tayari mashahidi watatu wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi  katika kesi hiyo akiwamo Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Urafiki, mrakibu wa Polisi (SP) Batseba Kasanga.

Katika kesi ya msingi, inadaiwa kuwa Julai 3, 2017 katika Makao Makuu ya Chadema, mtaa wa Ufipa wilaya ya Kinondoni,  Mdee anadaiwa kutamka maneno dhidi ya  Rais Magufuli kuwa  “anaongea hovyohovyo , anatakiwa  afungwe breki”  na kwamba kitendo hicho kingeweza  kusababisha uvunjifu wa amani.

Mdee alifikishwa kwa mara ya kwanza Kisutu Julai 10, 2017.