Ndesamburo kuwania uenyekiti Chadema kanda ya kaskazini

Mbunge wa zamani wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo

Muktasari:

  • Katika uchaguzi huo utakaofanyika kesho jijini Tanga, Ndesamburo anachuana na Daniel Porokwa.
  • Katibu wa Chadema wa kanda hiyo, Aman Golugwa alisema jana kuwa nafasi ya makamu mwenyekiti inawaniwa na wabunge wa Viti Maalumu Cecilia Pareso na Anna Gideria.

Arusha. Mbunge wa zamani wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo ni miongoni mwa makada wawili wa Chadema waliojitokeza kuwania uenyekiti wa chama hicho kanda ya kaskazini.

Katika uchaguzi huo utakaofanyika kesho jijini Tanga, Ndesamburo anachuana na Daniel Porokwa.

Katibu wa Chadema wa kanda hiyo, Aman Golugwa alisema jana kuwa nafasi ya makamu mwenyekiti inawaniwa na wabunge wa Viti Maalumu Cecilia Pareso na Anna Gideria.

Alisema nafasi ya mweka hazina wa kanda ya kaskazini inawaniwa na mbunge wa Viti Maalumu, Grace Kihwelu na mwenyekiti wa halmashauri ya Rombo, Evarist Silayo.

Katika uchaguzi huo, pia watachaguliwa mwenyekiti wa wabunge wa Chadema kanda ya kaskazini, nafasi inayowaniwa na Julius Kalanga (Monduli), Lucy Owenya (Viti Maalumu), Pauline Gekul (Babati Mjini) na Joseph Selasini (Rombo) ambaye anatetea nafasi hiyo.

Golugwa alisema nafasi ya katibu wa wabunge inagombewa na Yosaja Komba. Alisema mwisho wa kuchukua na kurejesha fomu ni leo saa 11:00 jioni.

Wakati huohuo, kamati kuu ya Chadema inakutana leo jijini Tanga, baada ya kuhitimisha ziara ya kukiimarisha chama hicho katika majimbo yote 35 ya kanda ya kaskazini.

Golugwa alisema kikao hicho kilitanguliwa na ziara za wajumbe wa kamati kuu katika majimbo hayo. “Ziara ilichukua siku nne, tulikuwa na timu nne mkoa wa Tanga, timu tatu mkoa wa Kilimanjaro, timu mbili Arusha na Manyara.”