VIDEO: Ndugai akerwa samaki kupimwa na ‘futi’ bungeni, Mpina aomba radhi

Spika wa Bunge, Job Ndugai

Muktasari:

  • Ndugai alitoa kauli hiyo jana baada ya kutangaza kumsamehe Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ambaye aliwasilisha maelezo ya Serikali kuhusu kilichotokea juzi, huku wabunge wakimtaka waziri huyo kujitathimini.

Dodoma. Spika wa Bunge, Job Ndugai ameelekeza masikitiko yake kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa kitendo cha maofisa wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuingia kwenye mgahawa uliopo bungeni pasipo taarifa na kuanza kupima samaki akisema kilichofanyika ni dharau.

Ndugai alitoa kauli hiyo jana baada ya kutangaza kumsamehe Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ambaye aliwasilisha maelezo ya Serikali kuhusu kilichotokea juzi, huku wabunge wakimtaka waziri huyo kujitathimini.

Mpina alitoa maelezo akitekeleza agizo la Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alilolitoa juzi jioni akihitimisha hoja iliyotolewa na mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), Peter Serukamba kuhusu hatua ya maofisa wa wizara kufanya kitendo hicho.

Hoja hiyo ilijadiliwa na wabunge 10 waliolaani kitendo hicho, baadhi wakimtaka Waziri Mpina na maofisa hao kuwajibishwa na Bunge.

Wabunge waliounga mkono hoja ya Serukamba ya kutaka kuwajibishwa kwa waziri huyo na maofisa waliopima samaki ni Abdallah Mtolea (Temeke-CUF), Rashidi Shangazi (Mlalo-CCM), Venance Mwamoto (Kilolo-CCM), Almasi Maige (Tabora Kaskazini-CCM), Zuberi Kuchauka (Liwale-CUF), Dk Immaculate Sware (Viti Maalumu-Chadema), John Kadutu (Ulyankulu-CCM), Dunstan Kitandula (Mkinga-CCM), Cecilia Paresso (Viti Maalum-Chadema) na Joseph Selasini (Rombo-Chadema).

Maelezo ya Serikali

Waziri Mpina aliliomba radhi Bunge na wabunge kwa kile kilichotokea akisema hakufanya hivyo kwa nia mbaya ingawa utekelezaji wa operesheni sangara utaendelea.

Alisema Juni 19 akiwa katika mgahawa wa Bunge aliona samaki aina ya sato akahofu wako chini ya sentimita 25 na kuamua kumwagiza katibu wake kwamba wakaguzi wakajiridhishe na samaki hao.

Alisema wakaguzi walimhoji muuzaji mgahawa ambaye alikiri kwamba walikuwa chini ya sentimita 25, “Napenda kukiri kwamba watumishi katika kutekeleza kazi hiyo waliingia bila kibali, kupima chakula kilichopikwa na kwa taratibu hizo wizara inaliomba radhi Bunge lako tukufu na wewe mwenyewe,” alisema Mpina.

Alisema, “Wizara yangu haikuwa na nia mbaya na ninaomba radhi kwa kutokufuata utaratibu na ninaomba Bunge liendelee kuunga mkono juhudi hizi.”

Msamaha wa Spika

Baada ya kauli hiyo, Spika Ndugai alisema, “Tumshukuru waziri kwa maelezo aliyoyatoa, lakini Waziri Mkuu tunasikitishwa sana na kilichotokea. Sisi si Bunge pekee duniani, sisi ni jumuiya ya kimataifa, wenzetu wakisikia kuna waziri na maofisa walichofanya ni dharau ya juu sana.

“Hata kunapokuwa na kosa la jinai limefanyika katika eneo la Bunge, RPC (Kamanda wa Polisi wa Mkoa) ana wajibu wa kunijulisha na sisi hatulindi wahalifu lakini lazima tujulishane,” alisema Spika akionekana mwenye kuchukizwa na tukio hilo, “Mtu akinunua samaki kilo 100, kwa akili ya kawaida, watu wananunua kwa kilo, hawanunui kwa futi, halafu samaki mwenyewe kapikwa, amekwisha kuwa kitoweo, sasa hii sheria ya kupima kitoweo! Itabidi hizi sheria tuzisome sana, yaani samaki mbichi amevuliwa huko atafika Dodoma kwa muda gani, bado urefu ni uleule?

“Wapimaji wale wa wizara wanapima mikono haina hata glovu, mikono wazi, wanashikashika, si wao peke yao, wamealika na waandishi wa habari, yaani ni kama mpango fulani wa kuliweka Bunge kusipostahili, kwa hiyo aah! Kwa kawaida naomba tukubaliane nami, ukiwa umekasirika sana unapaswa kusamehe,” alisema.

Wabunge wamshukia waziri

Mbunge wa Geita (CCM), Joseph Musukuma akichangia Bajeti ya Serikali ya mwaka 2018/19 bungeni jana alimtaka Waziri Mpina kujitafakari na kung’atuka madarakani.

Alisema, “Nilikamatwa na samaki katika basi langu, tukaombwa rula, kwa mara ya kwanza Wagogo watani zangu wana akili kubwa sana, ulichokifanya kusamehe kwa kusema ukichukizwa unasamehe waziri sasa ajitafakari.

“Mheshimiwa Spika, kweli nimeamini Wagogo, mtu amekuudhi unasamehe, wizara hii tumekuwa na mawaziri watano madokta, lakini leo tumeleta mgambo. Sijui shule ya aina gani? Ni vizuri tukakaguliwa vyeti, mtu ana elimu ya kuungaunga, yeye amekiri sijui hajui kwamba anakosea. Huu urais utakuja kututokea puani hasa sisi Wasukuma, tumeamua kunyamaza kumwachia Mungu apambane naye.”

Baada ya kumaliza kuchangia, Ndugai alisema, “Nikichukua samaki mmoja na kumweka pale ili wabunge wapime kila mmoja atakuja na majibu yake na ukipima lazima uje na majibu yake, yaani tunabishania sentimita moja kweli? Tunapotunga sheria, tunatunga kwa umakini.”

Katika viwanja vya Bunge, wabunge Abdallah Bulembo (Kuteliwa), Goodluck Mlinga (Ulanga-CCM), Ryoba Chacha (Serengeti-Chadema), James Mbatia (Vunjo-NCCR-Mageuzi) walizungumzia msamaha wa Spika Ndugai wakisema kauli hiyo inapaswa kumfikirisha Waziri Mpina.

“Spika ametumia busara tu ila waziri anapaswa kujiuzulu tu kwani atakosa ushirikiano kutoka kwetu wabunge,” alisema Mlinga.

Bulembo alisema, “Tunaheshimu kauli ya Spika. Kitendo kile bora kimekuja hapa ili kutuonyesha jinsi wananchi wetu wanavyoteseka huko, ni funzo kwetu. Waziri anapaswa kujiuliza hizi changamoto zinazojitokeza katika wizara yake, anapaswa kukaa chini na kuangalia kwa makini.”

Chacha alikwenda mbali zaidi akieleza, “Alichokisema Spika Ndugai ni kauli ya mtu mzima, ina maana yake, kwamba Rais achukue hatua.”

Mbatia alisema Spika hakupaswa kuichukulia binafsi, kwani kitendo kile kimewaudhi wabunge na kuuchafua mhimili huo na kilichopaswa kufanyika ni Bunge kuazimia kwa kauli moja.