Ndugai awaambia wabunge wakiikataa bajeti, Rais atavunja Bunge

Spika wa Bunge, Job Ndugai akimsikiliza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako alipokuwa akijibu baadhi ya hoja zilizotolewa katika mjadala wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Spika amewasisitizia wabunge wote kuwapo bungeni saa 11 huku akiwatahadharisha kuwa baadhi yao wakirudishwa majimboni hawarudi 

Dodoma. Spika wa Bunge Job Ndugai amesema kama wabunge wataipigia kura ya hapana Bajeti ya Serikali ya mwaka 2018/19, Rais atalivunja Bunge.

Spika Ndugai ametoa kauli hiyo leo asubuhi bungeni Juni 26, 2018 wakati akitoa maelezo ya kile kitakachofanyika leo saa 11 jioni ya kuipitisha bajeti.

“Endapo mlio wengi mtaikataa Bajeti ya Serikali, Bunge hili Rais atalivunja haraka,” amesema Spika Ndugai.

Baada ya kauli hiyo, minong’ono ya kutoka pande zote za wabunge ilisikika. Spika Ndugai hakuishi hapo, akasema tena:

 “Na baadhi yenu, mkirudishwa majimboni hamrudi kwa hiyo akili za kuambiwa changanya na zako.”

Amewaomba wabunge wote kuwapo bungeni ifikapo saa 11 jioni huku akisisitiza kwamba mbunge hapigi kura kwa jambo moja, bali ni kwa mfuko wote wa bajeti, kwa hiyo ni vizuri wananchi wakaelewa.

Katika hatua nyingine, Spika Ndugai amesema kuanzia sasa bendi ya muziki ya polisi, (Brass Band) itaingia bungeni kuongoza wimbo wa Taifa kabla na baada ya kikao cha Bunge kuanza.