Ndugulile apiga ‘stop’ uuzwaji vifaa vya kupimia Ukimwi

Muktasari:

Asema sheria hairuhusu mtu binafsi kujipima


Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile amepiga marufuku uuzwaji wa vifaa vya kupimia virusi vya Ukimwi kwa watu binafsi.

Naibu waziri huyo amesema hatua hiyo inatokana na sheria za nchi kutoruhusu mtu kujipima mwenyewe.

Hayo ameyasema leo Agosti 20, 2018 katika hafla ya kukabidhiwa cheti cha ubora wa kimataifa (ISO) kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Ndugulile amesema kwa mujibu wa sheria iliyopo sasa inaruhusu mtu kupimwa virusi vya Ukimwi na mtaalamu au mtoa huduma kutoka kituo cha afya na si vinginevyo.

"Hivi sasa bado tuko katika hatua ya kubadilisha sheria ili tuweze kuruhusu watu kujipima wenyewe lakini hii itakuwa baada ya majaribio yanayofanyika katika baadhi ya maeneo kuonyesha matokeo chanya," amesema Ndugulile

"Kwa hiyo basi naziagiza taasisi zangu kuhakikisha kuwa zinadhibiti uuzwaji holela wa vifaa hivi katika maduka ya dawa kote nchini," ameongeza.