Nemc yatakiwa kuwatumia Suma-JKT kufanya ukaguzi wa vyeti

Ushauri huo ulitolewa juzi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa Chama cha Wataalamu wa Mazingira.

Muktasari:

  • Ushauri huo ulitolewa juzi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa Chama cha Wataalamu wa Mazingira.
  • Makamba alisema asilimia 20 ya miradi iliyofikiwa na kufanyiwa ukaguzi wa vyeti vya athari za mazingira ni ndogo, hivyo ni lazima Nemc iongeze kasi katika mchakato huo.

Dar es Salaam. Serikali imelishauri Baraza la Taifa la Hifadhi na  Usimamizi wa Mazingira (Nemc), kuajiri  askari wa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (Suma-JKT) kufanya ukaguzi wa vyeti vya athari za mazingira katika miradi mbalimbali.

Ushauri huo ulitolewa juzi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa Chama cha Wataalamu wa Mazingira.

Makamba alisema asilimia 20 ya miradi iliyofikiwa na kufanyiwa ukaguzi wa vyeti vya athari za mazingira ni ndogo, hivyo ni lazima Nemc iongeze kasi katika mchakato huo.

Alisema kuna vijana wengi wa JKT waliomaliza mafunzo ambao wakiajiriwa watatoa msaada wa kufanya doria katika miradi na kukagua vyeti vya athari za mazingira.

“Wachukueni vijana hawa hata kama 1,000 au 2,000 na kuwapa mafunzo ya namna gani wataweza kufanya shughuli hii. Nawaambia mkifanya hivi nchi nzima itawajua Nemc ni nani. Ndoto yangu ni kuiona Nemc ikiwa na meno. Kila mtu akiisikia aiogope tofauti na sasa mtu akiisikia anatuma ujumbe mfupi tukutane ‘samaki samaki’,” alisema Makamba na kuibua kicheko kwa wataalamu hao.