Nida kuingia gharama upya

Muktasari:

Wananchi watakiwa kutunza vitambulisho vyao kuepuka gharama

Dar es Salaam. Serikali italazimika kuingia gharama ya kuchapisha vitambulisho vipya vyenye saini, baada ya vilivyopo kuondolewa kwenye matumizi.

Tayari, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), imetangaza kuanza kutoa vitambulisho vipya vya Taifa, kuanzia kesho kwa wananchi wote waliokamilisha taratibu za usajili na utambuzi.

Taratibu hizo ni kuchukuliwa alama za kibaiolojia zikiwamo za vidole, picha na saini ya kielektroniki.

Utekelezaji wa mabadiliko hayo unamaanisha kuwa Nida italazimika kuchapisha vitambulisho vipya, ambao utaiingiza kwenye gharama za kadi na uchapishaji. Taarifa iliyotolewa jana na Nida inaeleza kuwa, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wake, Andrew Massawe alisema kwa sasa vitambulisho vyote vitaendelea kutumika.

“Mamlaka inakusudia kubadilisha vitambulisho vyote vya zamani visivyo na saini, ila kwa sasa vitambulisho vya zamani vitaendelea kutumika sambamba na vipya wakati taratibu za kuvibadilisha zikiendelea,” alisema.

Massawe alibainisha kuwa kutokana na uwapo wa njia nyingi na salama za kusoma taarifa za mwombaji zilizomo ndani ya kifaa maalumu kilichofichwa kwenye kadi ya mtumiaji (chip), ndiyo maana vitambulisho vya zamani vitaendelea kutumika katika huduma mbalimbali.

Mkurugenzi huyo ambaye aliteuliwa Agosti na Rais John Magufuli ili kushika nafasi hiyo, alisema hivi sasa vitambulisho vya Taifa vimeanza kutumika kwa baadhi ya huduma nchini, hususan kwenye benki kwa ajili ya kufungua akaunti na kuthibitisha taarifa za mtu kabla ya kupatiwa huduma.

Kuhusu kuanza kutoa vitambulisho vipya vyenye saini, Massawe alisema vitaanza kutolewa katika ofisi zote za Nida. Ofisi hizo zipo za wilaya zilizoanza usajili (Tanzania na Zanzibar) na mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara, Morogoro, Tanga, Arusha, Kilimanjaro, na Ruvuma.

“Waombaji wote ambao vitambulisho vyao vipo tayari watatumiwa ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) katika simu zao za kiganjani, kufahamishwa kufika vituo vya usajili kuvichukua,” alisema.

Kuhusu wananchi ambao hawakuwahi kusajiliwa, Massawe alitoa rai kuendelea kujitokeza kusajiliwa kwenye mikoa ambayo tayari ina ofisi za usajili ili kupata vitambulisho vya Taifa.