Nyongeza ya mshahara Zanzibar mwezi ujao

Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein

Muktasari:

Dk Shein alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari Ikulu mjini hapa, ikiwa ni sehemu ya kusherehekea mwaka mmoja tangu alipoapishwa kushika wadhifa huo.

Zanzibar. Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema kima cha chini cha mshahara cha Sh300,000 kwa wafanyakazi wa Serikali kitaanza kulipwa mwenzi ujao.

Dk Shein alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari Ikulu mjini hapa, ikiwa ni sehemu ya kusherehekea mwaka mmoja tangu alipoapishwa kushika wadhifa huo.

Alisema katika kampeni za uchaguzi aliahidi akiingia madarakani ndani ya mwaka mmoja ataongeza kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi ili kwenda sambamba na mabadiliko ya hali ya maisha.

Rais alisema ahadi hiyo iko palepale na kuwataka wafanyakazi wasiwe na wasiwasi. Kima hicho kimepanda mara mbili kutoka Sh150,000 za sasa.

Alisema Serikali itaendelea kuweka mikakati ya kukusanya kodi ili kutoa fursa zaidi katika kuwaletea maendeleo wananchi.

Alisema uchumi wa Zanzibar umekua kwa asilimia 6.6 katika kipindi chake cha uongozi, kiwango ambacho kimempa faraja.