VIDEO-Msanii Jebby aliyetamba na ‘Swahiba’ afariki

Muktasari:

Jebby alikuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.

Msanii Jeneby Omari maarufu Jebby, aliyevuma na kibao cha Swahiba amefariki dunia.

Jebby amefariki dunia leo Aprili 22, 2018 saa tisa alasiri akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.

Khamis Omari, ambaye ni mdogo wa marehemu ameieleza MCL Digital kwamba ndugu yake alianza kuugua tangu Januari, 2018.

Amesema hali yake ilipozidi kuwa mbaya ndipo alikwenda Dodoma.

“Alianza kuuugua akiwa mkoani Iringa na hali ilipokuwa mbaya nilimchukua na kumleta Dodoma,” amesema.

Khamis amesema nduguye alikuwa akipingukiwa damu na kuvimba bandama.

Amesema Jebby atazikwa kesho Jumatatu Aprili 23, 2018 saa 10:00 jioni nyumbani kwa babu yake eneo la Area C mjini Dodoma.

Msanii Afande Sele akizungumza na MCL Digital amesema walizungumza na Jebby mwezi mmoja uliopita.

“Ni mwezi tu umepita Jebby alinipigia simu akaniambia anataka tufanye video ya wimbo wa Swahiba kwa kuwa ameona wasanii wengi wanatengeneza video za nyimbo zao za zamani. Nasikitika hatujalitekeleza hilo, leo napata taarifa kuwa amefariki,” amesema Afande Sele.

Mwisho.