Mkutano wa Odinga wavurugwa Meru

Muktasari:

Nasa walipofika walijaribu kuwatawanya hali iliyosababisha kuanza kurushiana mawe, mechi iliyodumu kwa saa kadhaa.

Nairobi, Kenya. Mkutano wa hadhara uliopangwa kuhutubiwa na Raila Odinga eneo la Laare, kaunti ya Meru umefutwa baada ya wafuasi wa chama cha Jubilee na muungano wa Nasa kutwangana.

Mkurugenzi wa mawasiliano wa ODM Philip Etale alithibitisha kwamba Odinga na makamanda wengine wa National Super Alliance (Nasa) watakuwa Meru kwa ajili ya kampeni yao ya “bila marekebisho hakuna uchaguzi”.

Mvutano ulikuwa mkali siku nzima baada ya wafuasi wa Jubilee na wale wa Nasa kutwangana kabla ya mkutano huo.

Vijana waliokuwa wakiimba nyimbo za Jubilee walichoma moto katika lango la kuingilia viwanja vya kiwanda cha kahawa cha Laare ambako mkutano ulikuwa umepangwa kufanyika.

Nasa walipofika walijaribu kuwatawanya hali iliyosababisha kuanza kurushiana mawe mechi iliyodumu kwa saa kadhaa.

Maofisa wa polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya wafuasi wa Jubilee waliokuwa wakizidi kuongezeka kuelekea kwenye uwanja wa mkutano.

Hata hivyo, kufikia saa 8:00 mchana ilikuwa wazi kwamba mkutano usingeweza kufanyika na ukawa umefutwa baada ya waandaaji kuanza kuondoa mahema, viti na zulia jekundu