Odinga afanya kampeni kuizuia Tume ya Uchaguzi

Muktasari:

  • Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari kwenye hoteli ya Panari jijini, kiongozi wa Nasa Raila Odinga amesema, kampeni hiyo ya nchi nzima itawatanabahisha Wakenya jinsi ambavyo IEBC haijajiandaa kusimamia uchaguzi wa kuaminika.

Muungano wa upinzani wa National Super Alliance (Nasa) umeanza rasmi kupiga kampeni za kuzuia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) kuandaa uchaguzi wa marudio kwa kura ya urais Oktoba 17.

Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari kwenye hoteli ya Panari jijini, kiongozi wa Nasa Raila Odinga amesema, kampeni hiyo ya nchi nzima itawatanabahisha Wakenya jinsi ambavyo IEBC haijajiandaa kusimamia uchaguzi wa kuaminika.

"IEBC kama ilivyo sasa haiwezi kusimamia uchaguzi ulio huru na haki Oktoba,” alisema Odinga juzi

Katika hatua nyingine, Marekani imetoa wito kwa Rais Uhuru Kenyatta na mpinzani wake Odinga kutatua masuala mazito kuelekea uchaguzi wa marudio.

Ofisa wa ngazi za juu katika utawala wa Rais Donald Trump alisema kuwa “macho yote yanekelekezwa Kenya” wakati huu ambao IEBC imewaita Rais Kenyatta na Odinga katika kikao muhimu kuhusu uchaguzi huo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Donald Yamamoto amesema Marekani imewasiliana na viongozi wa ngazi za juu wa kisiasa nchini na ikawaambia kwamba ulimwengu unaitazama Kenya.

Wito huo umetolewa katika kipindi ambacho IEBC inafikiria kusogeza mbele tarehe ya kura ya marudio kutokana na ombi la kampuni ya Safran Morpho. Kampuni hiyo ya Ufaransa wiki iliyopita iliwasilisha ripoti ya ukaguzi na ikaitaka IEBC isogeze tarehe ya uchaguzi hadi Oktoba 26 ili ipate muda wa kufanyia marekebisho mfumo wa mitambo yake.