Odinga amfariji Magufuli msiba wa dada yake

Muktasari:

  • Monica John Magufuli amezikwa leo katika kijiji cha Mlimani, kwenye makaburi ya familia.

Chato.  Waziri Mkuu Mstaafu wa Kenya Raila Odinga amehudhuria mazishi ya dada yake Rais John Magufuli aliyezikwa leo kijiji cha Mlimani, Chato.

Pamoja na Odinga, marais wastaafu wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan pia walihudhuria mazishi ya dada huyo wa Rais, Monica Joseph Magufuli.

Monica alifariki dunia Jumapili Agosti 19 katika Hospitali ya Bugando alikokuwa akipata matibabu.

Taarifa ya Ikulu iliyotolewa leo Agosti 21, imemkariri Mkurugenzi wa Idara ya Habari Mawasiliano wa Ikulu Gerson Msigwa kuwa, Misa ya mazishi ya imeongozwa na  Askofu wa Jimbo la Katoliki la Rulenge Mhashamu Severine Niwemuguzi aliyeambatana na maaskofu wengine saba.

Viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni , Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara  Philip Mangula, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Mawaziri, Wabunge, Viongozi Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama, Viongozi wa Madhehebu ya Dini, Viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wengine mbalimbali wa Mikoa, Wilaya, Taasisi, Idara na Kampuni.

Taarifa hiyo imesema marehemu Monica ameacha watoto tisa, mume na wajukuu 25.

Katika salamu zake Rais Magufuli amewashukuru viongozi na wananchi wote waliojitokeza kuungana na familia katika kumsindikiza dada yake katika safari yake ya mwisho.

“Mmetuonesha upendo mkubwa sana na kweli ujio wenu na kuungana nasi katika tukio hili mmetufariji sana, asante sana kwa upendo huu na Mungu awabariki sana, ”amesema  Magufuli.

Rais Magufuli amemuelezea Dada yake Monica kuwa alikuwa mtu mwenye upendo kwa familia nzima na alikuwa tegemeo kubwa la kumtunza mama yao mzazi  Suzana Ngolo Magufuli.

 “Alikubali kuondoka nyumbani kwa mumewe kwa zaidi ya miaka miwili na kurudi nyumbani kumlea mama yetu mzazi,” amesema Rais Magufuli katika taarifa yake.