Ofisi ya IGP kuhamia Dodoma mwezi ujao

IGP MANGU

Dar es Salaam.  Jeshi la  Polisi nchini limesema mwezi ujao litahamishia makao makuu yake mjini Dodoma, kuitikia agizo lililotolewa na Rais John Magufuli.

“Agosti tunahamia Dodoma. Tutafanya hivyo kabla ya Waziri wa Mambo ya Ndani na Waziri Mkuu,” alisema Nsato Marijani, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa jeshi hilo alipozungumza na mwandishi wa gazeti hili.

Jitihada za wizara na taasisi za umma kuhamia Dodoma, zinatokana na tamko la Rais Magufuli kuwa Serikali yake itatekeleza ndoto ya siku nyingi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kuhamia kwenye mji huo uliopo katikati ya nchi.

Siku moja baadaye, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangaza kuhamia Dodoma ifikapo Septemba na aliwataka mawaziri kumfuata.

Kamishna Marijani alieleza jinsi mpango huo utakavyotekelezwa kwamba Mkuu wa Jeshi na makamishna kadhaa watatakiwa kuhamia Dodoma, huku baadhi wakibaki na kuendelea na majukumu yao kutokea jijini hapa.