Ole Sendeka amsifu Lowassa

Rais John Magufuli akisalimiana na Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa walipohudhuria Misa ya Jubilei ya Dhahabu ya Ndoa ya Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na Mama Anna Mkapa katika Kanisa la Mtakatifu Petro jijini Dar es Salaam juzi. Picha na Ikulu

Muktasari:

  • Sendeka asema anamfahamu kuwa ni muungwana na asingeweza kuacha kumsalimia JPM

Dar es Salaam. Msemaji wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Christopher Ole Sendeka amesema Edward Lowassa ni muungwana na kwamba asingeweza kuacha kumsalimia kwa kumpa mkono Rais John Magufuli.

Ole Sendeka amesema jana: “Namfahamu Lowassa ni muungwana hawezi kuacha kusalimiana kwa kupeana mkono na Rais. Wamekutana viongozi, Rais na waziri mkuu mstaafu hawawezi kuacha kusalimiana.”

Lowassa ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema aliyechuana na Rais Magufuli katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015 mwaka jana, juzi walikutana kwa mara ya kwanza na mpinzani wake huyo tangu kinyang’anyiro hicho kilipomalizika.

Viongozi hao walikutana kwenye misa ya jubilei ya dhahabu ya ndoa ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa na mkewe Anna katika Kanisa la Mtakatifu Petro.