Oman yaahidi kushiriki katika uwekezaji wa viwanda

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman Dkt. Mohamed Hamad Al Rumhy alipokutana na kufanya naye mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 18, 2017

 

Muktasari:

Oman imeahidi kuendeleza sekta ya gesi na mafuta na ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo.

Dar es Salaam. Oman imesema ipo tayari kuunga mkono juhudi za Tanzania kwa kuongeza uwekezaji katika viwanda, uzalishaji wa nishati, kuongeza thamani ya madini, kuendeleza sekta ya gesi na mafuta na ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo ili kukuza uchumi.

Mfalme wa Oman Mtukufu Sayyid Qaboos bin Said Al Said amemhakikishia hayo Rais John Magufuli wa Tanzania kupitia ujumbe uliowasilishwa na Waziri wa Mafuta na Gesi wa nchi hiyo, Dk Mohammed Hamad Al Rumhy, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Waziri huyo alifuatana na mwingine wa Uwekezaji, Salem Ben Nasser Al Ismaily na Naibu Waziri wa Utalii, Maitha Saif Majid.

Dk Rumhy ambaye ameongoza watu zaidi 300 waliokuja nchini kwa meli ya Mfalme wa Oman amesema ziara hiyo imelenga kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na nchi hiyo na hasa katika masuala ya uchumi.

Amesema Oman inabadilishana uzoefu na Tanzania kuhusu biashara ya mafuta na gesi, itajenga kiwanda kikubwa cha kuzalisha mbolea katika ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo, itajenga viwanda vya mazao na kuyanunua ya wakulima na itawekeza katika uchakataji wa madini ili kuongeza thamani.

Taarifa ya Ikulu imesema Rais Magufuli amemhakikishia kiongozi huyo kuwa Tanzania ipo tayari kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano na Oman.

Amemtaka Dk Rumhy kufikisha ujumbe kwa mfalme na wawekezaji wa Oman kuwa atafurahi kuona uwekezaji huo unaanza mara moja na Serikali itatoa ushirikiano wowote utakaohitajika kwa manufaa ya pande zote mbili.

Rais Magufuli ametaka Oman iongeze ushirikiano na Tanzania katika masuala ya utalii na usafiri wa anga, kuwekeza katika usindikaji wa nyama na uvuvi na ushirikiano katika kubadilishana wataalamu wa nyanja mbalimbali wakiwemo walimu wa lugha ya Kiswahili na Kiarabu.

Amemshukuru Mfalme wa Oman kwa msaada uliowezesha ujenzi wa visima vya maji 100 nchini.

Rais Magufuli amemuomba kuungana na Serikali katika safari yake ya kuhamia Dodoma kwa kujenga miundombinu itakayoweka kumbukumbu ya ushirikiano wa kidugu na kihistoria kati ya nchi hizi mbili.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk Suzan Kolimba.