PM: Nampongeza RC Kilimanjaro kwa kazi nzuri

Muktasari:

  • Jumatatu hii, Majaliwa alipiga marufuku usafirishaji wa mahindi alipokuwa mkoani humo kwa ajili ya sherehe za Sikukuu ya Eid el Fitr.

Dodoma. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira kwa kuyazuia malori zaidi ya 100 yaliyokuwa yanasafirisha mahindi nje ya nchi.

Jumatatu hii, Majaliwa alipiga marufuku usafirishaji wa mahindi alipokuwa mkoani humo kwa ajili ya sherehe za Sikukuu ya Eid el Fitr.

Baada ya agizo hilo, malori hayo yalikamatwa na kuzuiwa. Akijibu maswali ya papo kwa papo bungeni leo  ( Alhamisi) juu ya zuio hilo, Waziri Mkuu amesema uamuzi huo ni moja ya hatua za kuhakikisha Taifa linajihadhari na ukosefu wa chakula hasa ikizingatiwa kwamba kulikuwa na uhaba wa mvua mwaka jana.

"Nampongeza Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro pamoja na kamati yake ya ulinzi na usalama kwa kuyazuia malori hayo," amesema Majaliwa.

Pongezi hizo zimetolewa siku chache baada ya aliyekuwa mwenyekiti na mgombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 wa Chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mghwira kuteuliwa kushika wadhifa huo.