Pinda avikwa gogoro la RC, m’kiti CCM

Muktasari:

Mwenyekiti akanusha kuvamia adai kununua kwa watu mbalimbali

Tarime. Baada ya kuwapo mvutano kati ya Serikali mkoani Mara na CCM wilayani Tarime kuhusu mipaka ya hifadhi ya Serengeti, chama hicho kimeunda kamati ya watu wanne kutafuta chanzo na namna ya kuutatua.

Hivi karibuni ilisambaa video kwenye mitandao ya kijamii iliyomuonyesha mkuu wa mkoa wa Mara, Adam Malima na mwenyekiti wa CCM wilayani Tarime, Marwa Ngicho wakibishana kuhusu eneo hilo.

Kamati iliyoundwa na CCM inaongozwa na Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda; ikijumuisha mwenyekiti wa umoja wa wanawake (UWT), Gaudencia Kabaka; mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Kheri James; na mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Makongoro Nyerere.

Kamati hiyo ilikwenda eneo lenye mgogoro wilayani Tarime juzi ambako pamoja na mambo mengine ilikagua eneo la mpaka wa hifadhi na la wazi ambalo baadhi ya wananchi akiwamo Ngicho wanadaiwa kuvamia.

Akizungumza wakati wa ukaguzi, Pinda alisema suala la kuwapo eneo la wazi ni la miaka mingi na la kisheria, hivyo watu wote wanaoishi na kufanya shughuli hapo wataondolewa kwa misingi ya kisheria.

Pinda alisema watu hao walitakiwa kufuata utaratibu wa ununuzi wa ardhi ikiwamo kwenda halmashauri kujua kama maeneo hayo yanafaa kwa matumizi ya binadamu na kwamba, suala la sheria halina chama wala kiongozi.

Hata hivyo, Ngicho alikanusha kuvamia eneo akisema alilinunua kutoka kwa watu mbalimbali kwa lengo la kufanya shughuli za ufugaji na makazi.

Naye Makongoro aliwataka wananchi kuwa wapole: “Tumekuja kuangalia chanzo cha mgogoro huu kisha tumshauri mwenyekiti (Rais John Magufuli) cha kufanya ili kupata ufumbuzi wa kudumu.”