Polisi Tanzania, Msumbiji wakubaliana kupambana na wahalifu mipakani

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro  (kulia) na na Mkuu wa Polisi wa Msumbiji, Bernadino Rafael wakiweka saini katika mkataba wa ushirikiano baina ya nchi hizo mbili katika kupambana na kuzuia ugaidi na dawa za kulevya, jijini Dar es Salaam jana. Picha na Said Khamis

Muktasari:

    Wahalifu waliodhibitiwa katika maeneo ya Kibiti, Mkuranga na Rufiji sasa wamekimbilia Msumbiji

 Jeshi la Polisi nchini limetiliana saini mkataba wa makubaliano na Jeshi la Polisi la Msumbiji kushirikiana kupambana na uhalifu katika nchi hizo mbili, hasa maeneo ya mpakani.

Mkataba huo utahusisha kubadilishana taarifa, mbinu na uzoefu katika kupambana na ugaidi na dawa za kulevya ambazo zinaathiri nguvu kazi kwenye mataifa yao.

Akizungumza na vyombo vya habari jana kabla ya kusaini makubaliano hayo, Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP, Simon Sirro alisema wahalifu waliodhibitiwa katika maeneo ya Kibiti, Mkuranga na Rufiji sasa wamekimbilia Msumbiji.

Hata hivyo, aliwaonya wahalifu hao kwamba hata huko hawatakuwa salama kwa sababu Jeshi la Polisi Tanzania linashirikiana na Msumbuji katika kupambana na uhalifu kwa kubadilishana taarifa.

“Wale wahalifu waliokimbilia Msumbiji au Congo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC) hawako salama. Majeshi yetu ya polisi yanashirikiana, ndiyo maana leo (jana) tulitiliana saini makubaliano ya ushirikiano,” alisema Sirro.

Aliwataka wahalifu hao waliokimbilia Msumbiji kuachana na uhalifu kwa sababu wakiendelea watakamatwa kwa ushirikiano wa majeshi hayo.

Mkuu wa Jeshi la Polisi la Msumbiji, Bernardino Rafael alisema kwamba nchi yake inakabiliwa na wahalifu kutoka nchi nyingine, hivyo makubaliano hayo yatasaidia kupunguza uhalifu.

Alisema wanataka kudhibiti mipaka yao dhidi ya wahalifu hao ambao wanahatarisha amani katika nchi hiyo pamoja na nchi za jirani.

“Watu wenye ualbino wanauawa kwa imani za kishirikina na taarifa zinaonyesha wahalifu hao wanatoka mataifa mbalimbali. Tutashirikiana na Polisi Tanzania katika kubadilishana taarifa ili kukomesha mauaji hayo,” alisema Rafael.