Polisi Uganda wataka kushikilia

Muktasari:

Polisi wanasema baadhi ya makosa, kama vile ugaidi, yanahitaji uchunguzi kupata ushahidi na mashahidi kutoka nje ya mipaka. Mamlaka hiyo inahitaji kuungwa mkono na Bunge kwa kubadili Ibara ya 23 ya Katiba.

 Kampala, Uganda. Jeshi la Polisi linakabiliwa na ukinzani mkali dhidi ya pendekezo la kutaka kuwaruhusu maofisa wake kuwashikilia watuhumiwa wa uhalifu kwa zaidi ya siku mbili kabla ya kupewa dhamana au kufikishwa mahakamani.
Wakati polisi wanasema mabadiliko hayo yatawahusu watuhumiwa wanaohusishwa na ugaidi, wapinzani wanadai kwamba upo uwezekano hata watuhumiwa wa makossa madogo pia kushikiliwa kwa muda mrefu.
Polisi wanasema baadhi ya makosa, kama vile ugaidi, yanahitaji uchunguzi kupata ushahidi na mashahidi kutoka nje ya mipaka. Mamlaka hiyo inahitaji kuungwa mkono na Bunge kwa kubadili Ibara ya 23 ya Katiba ili polisi waweze kuwashikilia watuhumiwa wa ugaidi kwa siku kati ya saba na 14 kabla ya kufikishwa kortini.
Naibu msemaji wa Jeshi la Polisi, Patrick Onyango alisema wakati mwingine kuhakiki sampuli zilizopatikana katika maeneo ya uhalifu kunahitaji muda wa kutosha kwa sababu “sisi pia tunatumia uhakiki wa maabara za serikali nyingine. Pia wanahitaji muda.”
"Wakati mwingine wanasema, 'tumeshtushwa na sampuli ... hizi sampuli mnazotuletea,'" aliongeza. "Kwa hiyo tunawaomba wabunge, kwamba katika baadhi ya matukio wanapaswa kubadili katiba ili waturuhusu tuweze kukaa na watuhumiwa kwa walau zaidi ya saa 48."
Kabla ya pendekezo hilo kusonga mbele lazima liungwe mkono na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki za Binadamu. Mwenyekiti wa kamati hiyo Jova Kamateka ameonyesha shaka. Anasema wamevurunda sheria.