Polisi wakanusha kumkamata Bobi Wine

Muktasari:

  • Hakuna aliyemkamata,” alisisitiza IGP. “Tunamsindikiza tu na kumpatia ulinzi kama tulivyoahidi. Anakwenda nyumbani,” alisema IGP.

Kampala, Uganda. Polisi wametoa ufafanuzi wakidai kwamba hawakumkamata mbunge wa Kyadondo Mashariki Robert Kyagulanyi Sentamu kama ilivyoandikwa katika vyombo vya habari.
Waandishi vya vyombo mbalimbali vya habari walioshuhudia tukio la kukamatwa mbunge huyo aliyekuwa akitokea Marekani ambako alikwenda kwa ajili ya kupatiwa matibabu maalumu waliripoti kwamba alikamatwa na maofisa usalama muda mfupi baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Entebbe.
Dakika chache baadaye aliondoka akiwa kwenye gari la polisi kwa kasi.
Hata hivyo, Inspekta Jenerali wa Polisi, Martin Okoth Ochola alisema kwa ujumbe wa twitter kwamba mbunge huyo hakukamatwa kama ripoti zinavyosema.
“Hakuna aliyemkamata,” alisisitiza IGP. “Tunamsindikiza tu na kumpatia ulinzi kama ambavyo tuliahidi. Anakwenda nyumbani,” alisema IGP.
Polisi walisema Jumatano kwamba hawatamruhusu Bobi Wine kuwa na maandamano kutoka uwanja wa ndege na kwamba atasindikizwa hadi nyumbani kwake Magere.
Dakika chache baada ya saa 8:00 mchana msafara wa polisi ukitokea Entebbe ulionekana kwa sehemu eneo la Ntinda baadaye ulisafiri kwa kasi katika barabara ya Mbogo hadi Kiwatule kuelekea Najera.
Msafara huo ulikuwa umesheheni makumi ya magari ya doria, gari la kubebea wagonjwa na magari mengine yaliyokuwa na namba za usajili wa polisi. Taarifa zilisema baadaye kwamba mbunge huyo alizuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Kasangati.