Polisi walivyomdhibiti Bobi Wine uwanjani

Muktasari:

  • Kisha maofisa usalama walimwendesha kwa kasi hadi nyumbani kwake Magere katika juhudi za kukata mawasiliano na wafuasi wake waliokuwa wakimsubiri kumpokea katika barabara ya Entebbe na katikati ya jiji la Kampala.

Kampala, Uganda. Polisi Alhamisi walimnyaka Mbunge wa Kyadondo Mashariki Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, akitoka kwenye ndege ya Shirika la Kenya (KQ) muda mfupi baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Entebbe.
Kisha maofisa usalama walimwendesha kwa kasi hadi nyumbani kwake Magere katika juhudi za kukata mawasiliano na wafuasi wake waliokuwa wakimsubiri kumpokea katika barabara ya Entebbe na katikati ya jiji la Kampala.
Nyumbani kwa Bobi Wine mji wa Magere katika wilaya ya Wakiso nje kidogo ya Kampala ni umbali wa maili 28 (kilomita 45) kutoka Entebbe.
Bobi Wine, ambaye anazidi kuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Rais Yoweri Museveni alikuwa akirejea nyumbani kutoka Marekani ambako alifuata matibabu maalumu baada ya kuteswa mikononi mwa usalama akiwa kizuizini.
Kyagulanyi na wanasiasa kadhaa wa upinzani walikamatwa na iliripotiwa kuwa walipigwa kinyama siku ya mwisho ya kampeni za uchaguzi mdogo jimbo la Arua mapema mwezi uliopita baada ya kutuhumiwa kwamba waulirushia mawe msafara wa Rais Museveni aliyekuwa ametoka kumpigia kampeni mgombea wa chama chake.
Jana, Kyagulanyi aliwasili kwenye uwanja wa Entebbe majira ya saa 7:00 mchana na mara baada ya kuchukuliwa na polisi alisafirishwa katika msafara uliokuwa na magari 14 ya doria hadi nyumbani kwake Magere kupitia barabara ya Entebbe-Kampala.

Vituko
Kyagulanyi amesema mara baada ya ndege aliyokuwa anasafiria kugusa ardhi katika Uwanja wa Entebbe, maofisa usalama walivamia ndani, wakamnyaka na kumweka kwa nguvu katika gari la polisi aina ya Prado lililokuwa likisubiri.
Alikalishwa hadi saa 9:00, karibu saa mbili tangu alipowasili ndipo Bobi Wine aliendeshwa huku akilindwa na Maofisa wa Kikosi cha Kupambana na Ugaidi.
Katika eneo la Abaita Ababiri, mwendo wa dakika 13 kwa gari (kilomita 7.1) katika barabara ya Entebbe-Kampala, askari walivamia soko la Abaita, wakapiga wafanyabiashara na wakalazimisha wafunge maduka hali iliyosimamisha shughuli za biashara.
Baada ya tukio la Abaita Ababiri, polisi na askari walifunga barabara kuruhusu msafara wa Kyagulanyi kupita haraka.

Nyumbani
Akiwa nyumbani, mwanamuziki huyo aliyegeuka mwanasiasa alisema namna ambavyo alidhibitiwa ni kielelezo cha jinsi serikali ilivyodhamiria kuwaweka Waganda katika utumwa.
 “Walinipokonya paspoti na nyaraka nyingine. Wala sijui ziko wapi. Waliniendesha hadi hapa (nyumbani). Nitaendeleza mapambano kuanzia nilipoishia,” alisema Kyagulanyi akiwa nyumbani kwake.
“Siko tayari kwenda uhamishoni. Nilizaliwa hapa na nitabaki hapa,” aliongeza.