Polisi wamwagwa hukumu za ubunge Kilombero, Mlimba

Muktasari:

Mbali na hatua hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe amepiga marufuku mikusanyiko ya watu katika mji wa Ifakara wakati na baada ya kusoma kwa hukumu hiyo kwa kuwa inaweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Morogoro/Tanga. Jeshi la Polisi mkoani Morogoro limeimarisha ulinzi katika Wilaya ya Kilombero wakati Mahakama Kuu itakapotoa hukumu ya kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa wabunge wa majimbo ya Kilombero na Mlimba leo.

Mbali na hatua hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe amepiga marufuku mikusanyiko ya watu katika mji wa Ifakara wakati na baada ya kusoma kwa hukumu hiyo kwa kuwa inaweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Dk Kebwe alisema ana imani kuwa hukumu hiyo itasomwa katika hali ya utulivu na hata baada ya kusomwa kila upande utaridhishwa na uamuzi ya Mahakama.

“Mahakama ni mhimili usioingiliwa, lazima tuheshimu sheria na pia maamuzi ya Mahakama, nawasihi viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa kuwatuliza mashabiki wao na endapo hawataridhishwa na hukumu, basi wafuate sheria kwa kukata rufaa na si kuchochea vurugu,” alisema.

Katika Jimbo la Kilombero, aliyekuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM, Assenga Damian alifungua kesi dhidi ya aliyeshinda, Peter Lijualikali wa Chadema kwa madai kuwa matokeo yaliyotangazwa hayakuwa halali.

Kadhalika, aliyekuwa mgombea ubunge katika Jimbo la Mlimba kupitia CCM, Godwin Emmanuel alipinga ushindi wa Suzan Kiwanga pia wa Chadema kwa madai mbalimbali ya ukiukaji wa taratibu. Wakati Dk Kebwe akitoa rai hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei amewataka wananchi wa Ifakara kutolijaribu jeshi la polisi kwa kufanya vitendo vya vurugu wakati hukumu hiyo ikisomwa.

Alisema jeshi hilo limejipanga kwa kupeleka askari wa kutosha na vitendea kazi vya kisasa kupambana na yeyote atakayeleta vurugu.

Matei alisema hakuna mtu au kikundi chochote kitakachoachwa kifanye vurugu, uchochezi au kuhatarisha amani wakati wa kusomwa kwa hukumu hiyo.

Pangani CCM kidedea

Katika hatua nyingine, Mahakama Kuu jana ilimpa ushindi Mbunge wa Pangani (CCM), Jumaa Awesso ilipotupilia mbali madai yaliyokuwa yamewasilishwa na Amina Mwidau (CUF) ya kupinga matokeo ya Ubunge Oktoba mwaka jana.

Hukumu hiyo ya saa 3.16 ilitolewa na Jaji Patricia Fikirini akisema mlalamikaji haukuweza kutoa ushahidi wenye kujikita katika hoja ya msingi ya kesi yenyewe.

Alisema mashahidi wote wa mlalamikaji pamoja na mawakili wake, Mashaka Ngole na Twaha Taslima hawakuthibitisha kama madai yaliyowasilishwa mahakamani hapo hayana shaka.

“Ushahidi uliotolewa kuuhusisha upande wa mlalamikiwa na matamshi ya matusi, kishirikina na ubaguzi wa kijinsia haukuweza kuthibitisha kama yangeweza kuathiri matokeo ya uchaguzi,” alisema Jaji Fikirini.

Akizungumza baada ya hukumu hiyo, Wakili Ngole

alisema hakuridhishwa na hukumu hiyo kwa sababu hoja zilizotolewa na jaji hazikuzingatia malalamiko yaliyowasilishwa.

Wakili wa Aweso, Warehema Singano alieleza kuridhishwa na hukumu hiyo na kuutaka upande wa mlalamikaji kukubali matokeo na kujipanga kwa Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Imeandikwa na Hamida Shariff, Burhani Yakub na Raisa Said.