Monday, February 19, 2018

VIDEO-Polisi wazingira ofisi za CUF Zanzibar, viongozi washangazwa

By Muhammed Khamis na Haji Mtumwa mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Polisi Zanzibar jana ilizingira ofisi za makao makuu ya CUF zilizopo Mtendeni mjini Unguja kwa kile kilichoelezwa kuwepo wa hali ya sintofahamu kwenye ofisi hizo.

Hata hivyo, mkurugenzi wa Habari wa CUF, Salim Abdallah Bimani alisema alishangazwa na uwepo wa taarifa za ugomvi kwenye ofisi hizo akisema hazina ukweli.

Akizungumza na Mwananchi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Hassan Nassir Ali alisema walifika katika ofisi hizo saa kumi na mbili jioni.

Kamanda Hassan alisema hatua hiyo imetokana na uwepo wa taarifa kutoka vyanzo mbalimbali kuhusu hali ya sintofahamu kwa baadhi ya viongozi wa chama hicho ndani ya ofisi hizo.

Alisema wakiwa walinzi wa amani walilazimika kuzingira ofisi hizo ili kuweka utulivu na hawakuwa na dhamira mbaya.

Kamanda Hassan alisema anaamini wapo baadhi ya watu wanaweza kufikiria polisi walikwenda kuvamia lakini hilo halikuwa lengo lao, bali kuhakikisha amani inakuwepo.

Alitoa wito kwa wananchi kuendelea na shughuli zao kama kawaida bila ya taharuki.

“Lazima vyama vya siasa na jamii kwa jumla vitambue nchi inalindwa kwa misingi ya sheria hivyo ni wajibu wetu kila mmoja kufuata sheria bila ya kushurutishwa,” alisema.

Mkurugenzi wa Habari wa CUF, Bimani alisema anashangazwa na uwepo wa taarifa za ugomvi kwenye ofisi hizo.

Alisema iwapo kuna watu wamewapa polisi taarifa hizo basi wana nia mbaya ya kukichafua chama.

Bimani alitoa wito kwa wanachama na wananchi kwa jumla kuendelea kuwa watulivu.

Mwananchi aliyeshuhudia tukio hilo ambaye hakupenda kutajwa jina gazetini alisema aliona kundi la askari wenye silaha wakizunguka eneo la ofisi hizo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro ameandika katika Facebook kwamba polisi wana ajenda mbili; kuishikilia kimabavu ofisi hiyo au kuweka vitu vya hatari na kisha kuwakamata viongozi wa chama hicho.

-->