Polisi yaomba amani Sikukuu ya Eid El Fitri

Muktasari:

  • Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Mohamed Msangi (pichani) alisema kuwa wamejipanga kudhibiti uhalifu katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo na viunga vyake.

Yawataka waendesha bodaboda na watu wengine wenye nia ya kufanya uhalifu waache

Polisi mkoani Mwanza imewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo ili kuimalisha ulinzi wakati wa Sikukuu ya Eid El Fitri.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Mohamed Msangi (pichani) alisema kuwa wamejipanga kudhibiti uhalifu katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo na viunga vyake.

“Lakini niwaombe wananchi wenyewe wawe walinzi wa mali zao kwanza, sisi polisi tunaongeza nguvu katika jitihada zinazofanywa na wananchi wenyewe hivyo tunahitaji ushirikiano, maana sisi hatuwezi kufika maeneo yote kwa wakati mmoja,” alisema Msangi.

Kamanda Msangi aliwataka wazazi na walezi kutowaruhusu watoto kutembea peke yao barabarani, kwenda maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu bila uangalizi na wasiruhusiwe kabisa kwenda kwenye kumbi za starehe.

Hata hivyo, Kamanda Msangi alimtaka kila moja kutimiza wajibu wake kwa kufuata sheria bila shuruti.

“Madereva, waendesha bodaboda na watu wengine wenye nia ya kufanya uhalifu waache, ila kama kuna mtu atahitaji kushurutishwa nasi tupo tayari kufanya hivyo,” alisema.

Paul James mkazi wa Nyegezi aliwashauri wazazi kupunguza matumizi makubwa ya fedha msimu huu wa sikukuu na badala yake wajiwekee akiba.

“Maisha kwasasa ni magumu, wapo baadhi wanaofuja fedha wakati wa sikukuu kama hizi kisha baadaye wanaanza kuhangaika, hivyo ni vyema wakatambua kuwa baada ya sikukuu maisha lazima yaendelee,” alisema James

Mkazi mwingine wa Buhongwa, Matrona Marlow aliwataka wazazi kurudi nyumbani mapema wakati huu wa sikukuu.