RC ‘awavisha bomu’ maofisa elimu

Muktasari:

  •    Akatishwa tamaa na idadi ya wanafunzi walioripoti kidato cha kwanza

Wakati mkoa wa Pwani ukionyesha kupanda katika matokeo ya kidato cha pili mwaka jana kutoka nafasi ya 13 hadi ya tisa na nafasi ya 12 kutoka 15 kwa darasa la nne, hali ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza hairidhishi.

Kutokana na hali hiyo, mkuu wa mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo ametoa siku saba kwa maofisa elimu, wakuu wa sekondari kuhakikisha watoto wote waliopangiwa kidato cha kwanza mwaka huu kuripoti shuleni na iwapo watashindwa kutekeleza agizo hilo watakuwa wamejivua vyeo vyao.

Ndikilo alitoa tamko hilo Januari 18 katika Sekondari ya Mboga alipotembelea kujionea hali halisi ya mahudhurio ya wanafunzi wa kidato cha kwanza na kuzungumza na maofisa elimu, wadau na watumishi wa halmashauri za Chalinze na Bagamoyo.

Katika ziara yake hiyo alibaini katika kipindi cha wiki mbili tangu shule zifunguliwe, mwitikio wa wanafunzi wa kidato cha kwanza walioripoti kwenye shule walizopangiwa siyo wa kuridhisha, kwani kwa mkoa mzima idadi ya waliyoripoti ni chini ya asilimia 51.

Ndikilo alitoa mfano wa taarifa aliyonayo kwa siku ya Januari 17 ni kuwa wanafunzi walioripoti kwa halmashauri ya Chalinze ni asilimia 50.6, Bagamoyo 43.4, Rufiji 75 na Mafia 86.7.

“Nimeamua kupita hapa Mboga baada ya kupata taarifa ya hali ya wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka huu kuripoti darasani mkoani kwetu hadi sasa hairidhishi, watoto wengi wapo nyumbani na nimejionea. Sasa natoa tamko ndani ya siku saba nataka wawepo darasani sitaki kisingizio chochote na tutawajibishana hata kuvuana vyeo,” alisema Ndikilo.

Pia, aliagiza vyombo vyote ya usalama kufanya msako wa nyumba kwa nyumba na wakimbaini mzazi au mlezi ana mtoto wa kidato cha kwanza ndani hajamruhusu kwenda shule akamatwe mara moja na afikishwe mahakamani.

Akizungumzia hali hiyo, mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete pamoja na mambo mengine alisema zipo changamoto zinazosababisha wanafunzi kuchelewa kuripoti walikopangiwamojawapo ni mgawanyo na mpango uliotumika wa wapi mwanafunzi aende mfano; wapo watoto wa Kata ya Bwilingu wamepangiwa kwenda Matipwili umbali wa zaidi ya kilomita nane.

Naye mkuu wa Sekondari ya Mboga, George Elias alieleza kuwa mpaka sasa kati ya wanafunzi 197 waliopangiwa hapo ni 102 sawa na asilimia 51 ndiyo wameripoti.

Katika mwaka 2017, wanafunzi 18,242 mkoani Pwani walifaulu sawa na asilimia 66.9 wote wamepangiwa shule mbalimbali.