Monday, September 10, 2018

RC Hapi agoma kuweka jiwe la msingi Zahanati ya Mgogolo

 

By Berdina Majinge,Mwananchi Bmajinge@Mwananchi.co.tz

Mufindi. Mkuu wa mkoa wa Iringa Ally Hapi amegoma kuweka jiwe la msingi katika kliniki ya mama na mtoto iliyopo katika zahanati ya Mgololo iliyojengwa chini ya kiwango.

Mkuu huyo ameshindwa kuweka jiwe la msingi hilo wakati akitembelea miradi ya maendeleo iliyopo katika tarafa ya Kasanga wilayani Mufindi kutokana na kutopata maelezo ya kutosha juu ya jengo hilo na gharama zilizotumika.

Amesema mradi huo wa kliniki una thamani ya Sh360 milioni ambazo zimetolewa na mwekezaji wa kiwanda cha karatasi Mufindi lakini jengo likionekana kuwa chini ya kiwango halifanani na thamani ya pesa.

“Nimeshindwa kuweka jiwe la msingi kwenye kliniki hii kutokana na fedha zilizotumika kushindwa kukidhi aina ya majengo yaliyojengwa katika kliniki hii hivyo nawaomba mrudie kupiga bajeti upya,” amesema.

Hali hiyo imekuja baada ya kusomewa taarifa ya ujenzi na kubaini thamani ya mradi na fedha zilizotolewa hazilingani na thamani ya majengo na kuwataka wahusika kuwasilisha mchoro ofisini kwake ili kujiridhisha kama thamani ya mradi inaendana na mradi wenyewe.

Hapi ametembelea ujenzi wa vyumba vya maabara katika Shule ya Sekondari Mgololo ambao umejengwa kwa msaada wa kiwanda cha karatasi Mufindi yenye thamani ya Sh 460 milioni.

Akisikiliza kero za wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Mabaoni, wananchi hao walimlalamikia mwekezaji wa kiwanda cha karatasi cha Mufindi kuwapora ardhi waliyokuwa wakimiliki kihalali bila kuwapa fidia yoyote hali inayowasababisha kukosa maeneo ya kujiendeleza kiuchumi.

Akizungumza mmoja wa wanakijiji hao, Yohana Nziku amesem, “kiwanda hiki kimekuwa kikitunyanyasa wanakijiji kwa kuchukua ardhi yetu bila kutulipa fidia na kudai ni eneo la mashamba ya miti ya kiwanda hicho jambo ambalo linatukwaza na wakati mwingine hatupewi hata fidia wala viwanja vingine vya kujenga makazi.”

Akijibu tuhuma hizo meneja wa kiwanda hicho, Gregory Chogo amesema maeneo hayo walipewa kihalalai na Serikali na wamekuwa wakilipa fidia kutokana na tathimini inayofanywa na Serikali.

Katika hilo, Hapi amebaini mashine za kutengenezea karatasi nyeupe zimezimwa na kufanya karatasi hizo kutozalishwa hali inayoikosesha Serikali mapato.

“Nataka kiwanda kianze kuzalisha karatasi nyeupe kuona mashine za kutengenezea karatasi nyeupe mimi kama mkuu wa mkoa sijaridhishwa na kuzimwa kwa mashine ya kutengenezea karatasi nyeupe zilizowekwa na Baba wa Taifa (Mwalimu Julius Nyerere) kwa gharama kubwa kuona hazifanyi kazi na tunanunua madaftari nchi nyingine wakati malighafi inatoka kiwandani kwetu,”amesema.

Amesema atahakikisha anaweka mkakati madhubuti kupitia viwanda vya mkoa wa Iringa vilivyokuwa vimekufa kufufuliwa na kuanza kufanya kazi, kwani kwa kufanya hivyo uchumi utapanda na vijana watapata ajira.

 

-->