RC Iringa awataka watimize wajibu wao

Muktasari:

Masenza ametoa agizo hilo leo Ijumaa wakati wa hafla ya uzinduzi wa zao la korosho uliyofanyika katika Kijiji cha Idodi Halmashauri ya Iringa.

Iringa. Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza amewataka maofisa ugani kutoka katika maeneo yanayolima zao la korosho wilayani Iringa kutimiza wajibu wao ili kuwezesha zao hilo kuzaa matunda yaliyokusudiwa.

Masenza ametoa agizo hilo leo Ijumaa wakati wa hafla ya uzinduzi wa zao la korosho uliyofanyika katika Kijiji cha Idodi Halmashauri ya Iringa.

Zao hilo jipya Iringa limeanzishwa wakati ambapo Mkoa umezindua kampeni ya uanzishwaji viwanda ijulikanayo kwa ‘Iringa yetu viwanda vyetu huku’ huku zao hilo jipya likitajwa kwa mwarubaini wa kuongeza viwanda vya kubangua korosho na kukuza uchumi wa mkoa huo.

“Tunataka mkoa ufanikiwe katika kilimo cha zao hili na ushauri wangu itungwe sheria ndogo itakayomlazimisha kila mkulima kushiriki katika kilimo hiki kinachotarajiwa pia kuchochea uanzishwaji wa viwanda vya kubangua korosho,” alisema Masenza na kuongeza:

“Lakini pia nataka kuona viongozi wa vijiji katika maeneo husika wanakuwa wa mfano kwa kuwa na mashamba darasa ambayo wananchi wengine watayatumia kujifunza.”