RC Mbeya: Watumishi wanashirikiana na wafanyabiashara kuhujumu mapato ya Serikali

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amesema kuna watumishi wanaoshirikiana na wafanyabiashara kuhujumu mapato ya Serikali mkoani hapa, kuapa kuwashughulikia kuanzia sasa

Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amesema kuna watumishi wanaoshirikiana na wafanyabiashara kuhujumu mapato ya Serikali mkoani hapa, kuapa kuwashughulikia kuanzia sasa.

Chalamila ametoa kauli hiyo leo Oktoba 9, 2018 wakati akizungumza na wakuu wa idara, wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa wilaya zote za Mkoa wa Mbeya katika kikao kazi  kilichofanyika mjini hapa.

Amesema kuna wafanyabiashara wanajiita ‘vidume’ na hawataki kulipa kodi na kila anapowaita kwa ajili ya kufanya nao mazungumzo wamekuwa na majibu yasiyofurahisha.

Amesema lazima afanye jambo kuonyesha kuwa Serikali ipo na haijaribiwi.

“Unawaita tuzungumze wanajibu ‘So arrogantly’ halafu wanam-copy barua Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa), Rais (John Magufuli) na makamu wa Rais (Samia Suluhu Hassan). Sasa ili kudhihirisha kwamba Serikali ipo, nimempigia simu Suleimani Jafo (Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa),” amesema.

“Nikampigia Waziri Mkuu nikawaambia mkisikia mlio tu nyie kaeni kimya. Kwa hiyo na nyie mkisikia mlio tulieni tu. Mjue tu wanaume wapo kwenye kazi za kawaida na sitaki kuulizwa.”

Amesisitiza, “ni shoo ambayo itaonekana…, mnasema Mbeya pagumu? Mbeya pagumu hakuna ugumu wagumu ni sisi wachache tuliojigeuza kuwa wezi kwa kushirikiana na wafanyabiashara kuhujumu. Na huu ndio ukweli kinashindikana vipi kama sheria zipo?”

Alisema tangu 2007 lilipoungua soko la Mwanjelwa, wafanyabiashara hawajawahi kulipa kodi na hata walipohamia soko la Sido, kwamba  hataweza kuvumilia suala hilo na atachukua hatua stahiki ambazo hatapenda kuona analalamikiwa kwa uamuzi wake.

“Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya haijakusanya kodi  katika soko la Mbalizi tangu mwaka 2016 mpaka leo, ukiwauliza kwa nini eti walipandishiwa kodi kidogo halafu wao (wafanyabiashara) wakapeleka mapingamizi yao mahakamani wakipinga kupandishiwa kodi  kwenye nyumba ya halmashauri,” amesema.

Amesema soko la Sido halijawahi kuingiza chochote kwenye halmashauri ya Jiji tangu mwaka 2007 lilipoungua soko la Mwanjelwa.

Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, Mariam Mtunguja amesema miaka ya nyuma Mkoa ulikuwa ukikusanya mapato kwa asilimia 80 lakini mwaka huu wamekusanya kwa asilimia 71.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika amesema, “mamlaka na madaraka vyote vinavyo hivyo nilikuwa nasubiria tu kauli yako mkuu wa mkoa, na sasa nakwenda kuchukua hatua dhidi ya wale wote ambao hawataki kulipa kodi.”